UHASAMA mkali wa kisiasa unaendelea kutokota katika Kaunti ya Migori kati ya Gavana Ochilo Ayacko na Mbunge wa Uriri Mark Nyamita ambao wote walichaguliwa kwa tiketi ya ODM mnamo 2022. Bw Nyamita tayari ametishia kuwa atahama ODM iwapo chama hicho kitampendelea Bw Ayacko katika mchujo. Ubabe kati ya wawili hao umefika kilele chake huku wafuasi wao wakitifuana kwenye mikutano ya umma na hafla za mazishi. Bw Ayacko anahudumu muhula wake wa kwanza kama gavana naye Bw Nyamita anahudumu muhula wa pili kama mbunge. Katika mahojiano na Taifa Leo , Bw Nyamita alisema kuwa atasaka hifadhi kwingine iwapo ODM itamchezea shere kwenye mchujo wake. Kauli yake sasa inaweka mchujo wa chama hicho kinachoongozwa na Dkt Oburu Oginga katika mizani baada ya kuandamwa na ukosefu wa uwazi katika chaguzi za nyuma. Bw Nyamita alijitosa kwenye siasa mnamo 2013 akiwa na umri wa miaka 32 akiwania ubunge wa Uriri lakini akashindwa. Anasema baada ya kuhudumu kama mbunge kwa mihula miwili, sasa ametosha kuwa gavana. Tayari amebuni kauli ‘Ochilo Byeee’ ambayo imechangamsha wafuasi wake na kuwakasirisha mahasimu wake kisiasa. “Gavana ana rasilimali lakini mimi nina mawazo kwa hivyo itakuwa ushindani kati ya rasilimali kutumika vibaya kupiga vita mawazo mazuri,” akasema Bw Nyamita. Alisema ameamua kuwania ugavana kutokana na utendakazi wa kuridhisha na ameahidi kubadilisha kaunti hiyo kiuchumi. “Siendei kiti hicho kwa sababu ya nguvu za ukoo wangu bali kuwatumikia watu wetu kupitia mawazo haya niliyo nayo. Nataka watu wanichague kwa sababu ya uchapakazi wangu ambao wanaweza kuona eneobunge langu na kwenye manifesto yangu,” akasema. Kwa mujibu wa mbunge huyo, kaunti hiyo imehiniwa maendeleo kutokana na uongozi mbaya. “Kile ambacho Migori inahitaji ni kiongozi ambaye atafanya juu chini kuhakikisha kuwa miradi inatekelezwa. Hiyo ndiyo nalenga kufanya,” akasema Bw Nyamita. Alisema kuwa sekta ya afya imedorora katika kaunti huku hospitali nyingi zikiwa hazina dawa. Pia alilalamika kuwa kaunti haina miundomsingi bora licha ya kwamba inapakana na Ziwa Viktoria na ina viwanda vya sukari pamoja na uchimbaji wa dhahabu kunoga. Akigusia ufanisi wake, Bw Nyamita alisema kuwa sekta ya elimu imeinuka sana katika eneobunge lake na atafanya hivyo katika kaunti nzima. Bw Nyamita alikuwa kati ya viongozi wa kwanza kutembelea ikulu baada ya ushindi wa Rais William Ruto. Kutokana na ziara hiyo, viongozi hao walishutumiwa na kurejelewa kama fuko na wenzao wa ODM ambao bado walikuwa wakilalamikia kura za Raila Odinga kuibwa. Mbunge huyo hadi leo hajutii ziara hiyo akisema alipata miradi mingi ambayo imekamilishwa na inawanufaisha wakazi. Miradi hiyo ni Hospitali ya Level Four ya Piny Owacho, Chuo cha Kiufundi cha Uriri ambacho sasa kina wanafunzi 3,000 na walimu 33. “Hata kama mambo yangejirudia, bado ningefanya hivyo. Hakukuwa na chochote kibaya kuenda Ikulu kumtembelea Rais William Ruto,” akasema.