Vita vya mabinamu vyatishia kugawa Mlima kwa mara ya kwanza tangu 1992

BAADHI ya wanasiasa sasa wanaendeleza shinikizo za kuhakikisha eneo la Mlima Kenya Mashariki linajitenga na lile la Magharibi na kuelekeza kura zake kwa kambi ya Rais William Ruto mnamo 2027. Kaunti zinazounda Mlima Kenya Mashariki ni Embu, Meru na Tharaka-Nithi. Wakazi wa ukanda huo wamekuwa wakipiga kura pamoja na wenzao wa jamii ya GEMA kutoka Mlima Kenya Magharibi. Magatuzi ya Mlima Kenya Magharibi ni Kirinyaga, Nyeri, Nyandarua, Murang’a, Kiambu, Laikipia na Nakuru. Tangu mfumo wa vyama vingi uanze kutumika mnamo 1992, eneo lote la Mlima Kenya limekuwa likielekeza kura zao mahala pamoja. Ni katika uchaguzi wa 1992 ambapo marehemu Mwai Kibaki na Kenneth Matiba waligawa kura za Mlima Kenya. Matiba ndiye aliyejizolea kura nyingi eneo hilo katika uchaguzi wa mwaka huo. Katika uchaguzi wa 2002, eneo hilo lilimpigia Bw Kibaki kura isipokuwa Kiambu ambapo Uhuru Kenyatta alitamba akiwania urais kupitia Kanu. Mara nyingi mwelekeo wa siasa za Magharibi ndio umekuwa ukifuatwa na ule wa Mashariki. Hata hivyo, huenda desturi hiyo ikaisha iwapo juhudi zinazoendelezwa na Waziri wa Utumishi wa Umma, Geoffrey Ruku na Gavana Cecily Mbarire zitafaulu. Wawili hao wanaotoka Kaunti ya Embu wako katika kambi ya Naibu wa Rais Prof Kithure Kindiki ambaye analenga kuwa mgombeaji mwenza wa Rais Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027. Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua naye amekuwa akijikita katika siasa za Mlima Kenya akilenga kura zote za eneo hilo bila kujali ni za mashariki au magharibi. “Mlima Kenya Mashariki lazima usimame kivyake na kulinda maslahi yake ya kiuchumi na kisiasa. Tugawanye mlima ikiwa italazimu na Mlima Kenya Mashariki utasimama kivyake,” akasema Bw Ruku mnamo Jumapili. Huku Bw Gachagua akilenga kuhakikisha Mlima Kenya unaelekeza kura zake kwa atakayewania kupitia upinzani, Prof Kindiki naye anajizatiti kupata uungwaji eneo hilo ili awe katika nafasi nzuri ya kuendelea kuwa naibu rais baada ya 2027. Bw Ruku alisema wakazi wa Mlima Kenya Mashariki wameumia kwa kipindi kirefu kwa kuwa wao hujumuishwa tu na wenzao upande wa magharibi, akidai hilo limesababisha wasipige hatua nzuri kimaendeleo. “Hatuwezi kuruhusu tuingizwe mfukoni na tutumike vibaya ilhali ni wenzetu ndio wananufaika,” akaongeza. Akihutubu Embu wikendi, Bw Ruku alisema fursa ya Prof Kindiki kushikilia wadhifa wa naibu rais ni ishara tosha kwamba wao wanaweza kuamua mustakabali wao wa kisiasa. Pia alimshutumu Bw Gachagua akidai anaendesha siasa za mgawanyiko, akisema kuwa yaliyo muhimu ni Mlima Kenya Mashariki pia kunufaika kwa miradi ya ustawi na kujinasua katika umaskini. Vilevile Bw Ruku alidai kuwa utawala wa Kenya Kwanza umefungua eneo hilo kimaendeleo na sasa bei ya chai na kahawa imepanda mno. Bi Mbarire alimuunga mkono Bw Ruku akisema kuwa wakati umefika ambapo Mlima Kenya Mashariki unastahili kuwa na mwelekeo wake wa kisiasa. “Hatutahusishwa kwenye siasa ambazo hazinufaishi watu wetu. Iwapo kuna haja itabidi tuamue mustakabali wetu wa kisiasa,” akasema Bi Mbarire. Prof Kindiki, Bi Mbarire na Bw Ruku walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba mwaniaji wa UDA Leo Muthende anashinda ubunge wa Mbeere Kaskazini katika uchaguzi mdogo mwezi jana. Hii ni licha ya Bw Gachagua na vinara wengine wa upinzani kukita kambi eneo hilo na kumvumisha Newton Karish wa DP. Kiongozi wa DP Justin Muturi na Seneta wa zamani wa Embu Lenny Kivuti pamoja na Mbunge wa Manyatta Gitonga Mukunji ni kati ya wanasiasa kutoka Mlima Kenya Mashariki ambao wako katika kambi ya Bw Gachagua.