Wito mtoto wa kiume pia alindwe dhidi ya maambukizi ya ukimwi

NAIBU Gavana wa Homa Bay, Oyugi Magwanga, sasa anataka wavulana walindwe kutokana na tabia zinazosababisha kuenea kwa virusi vya ukimwi. Bw Magwanga alisema kuwa jinsi wasichana wanavyolindwa, ndivyo pia mtoto wa kiume anastahili kufanyiwa. “Ndoa za mapema na maambukizi mapya huchangia kuhatarisha maisha ya watoto kuhusiana na ukimwi. Wazazi wanastahili kumakinika na kuwa na watoto wao nyakati zote,” akasema Bw Magwanga. Takwimu kutoka Baraza la Kitaifa la Kudhibiti Magonjwa ya Kuambukizana (NSDCC) zinaonyesha kuwa maambukizi ya ukimwi Homa Bay yamepungua kutoka asilimia 15.1 mnamo 2023 hadi asilimia 10.6 mnamo 2024. Maambukizi hayo ni ya juu ikilinganishwa na takwimu za kitaifa. Homa Bay ni kati ya kaunti tano ambazo zina viwango vya juu vya maambukizi ya ukimwi huku Nairobi ikiongoza nazo Migori, Kisumu na Busia zikifuata. Bw Magwanga alisema kuwa wakati huu ambapo shule zimefungwa ni vyema iwapo wazazi watamakinikia maslahi ya watoto wao. “Mzazi lazima afahamu mahali ambapo mtoto wake yupo. Isitoshe jinsi wasichana wanavyolindwa dhidi ya ubakaji ndivyo wavulana pia wanastahili kufanyiwa,” akasema Bw Magwanga. Naibu huyo wa gavana alikuwa akiongea katika Shule ya Upili ya God Ber kwenye Wadi ya Kakelo Kokanyo, Kaunti Ndogo ya Rachuonyo Mashariki. Alikuwa ameongoza mchango wa kukarabati miundomsingi ya shule hiyo.