Trump agonga Tanzania na marufuku makali

Rais wa Amerika Donald Trump amepiga marufuku raia wa Tanzania kuingia  nchi yake katika hatua inayoongeza masaibu kwa serikali ya Rais Samia Suluhu anayelaumiwa kwa ukandamizaji wa demokrasia na haki za binadamu. Katika tangazo lake,Trump alitaja udhaifu  wa serikali ya Tanzania katika mifumo ya uchunguzi, uhakiki na utoaji wa taarifa kuhusu raia wake. Katika tangazo la urais alilosaini Jumanne, Desemba 16, utawala wa Trump umeongeza Tanzania kwenye orodha ya mataifa ambayo raia wake wamewekewa  vizuizi kuingia Amerika, ukitaja viwango vya juu vya raia kuzidisha muda wa viza kama sababu kuu. “Leo, Rais Donald J. Trump alisaini tangazo linalopanua na kuimarisha vizuizi vya kuingia kwa raia wa nchi zilizo na mapungufu makubwa, ya kudumu na makali katika uchunguzi, uhakiki na utoaji wa taarifa, ili kulinda taifa dhidi ya vitisho vya usalama wa kitaifa na usalama wa umma,” ilisema sehemu ya tangazo hilo. “Vizuizi na masharti yaliyoanzishwa ni muhimu ili kuzuia kuingia kwa raia wa kigeni ambao Amerika haina taarifa za kutosha kutathmini hatari wanazoweza kuleta, kupata ushirikiano wa serikali za kigeni, kutekeleza sheria za uhamiaji, na kutimiza malengo muhimu ya sera za kigeni na usalama wa taifa.” Kwa mujibu wa takwimu za Amerika, Watanzania wanaosafiri kwa viza za B-1/B-2 wana kiwango cha kuzidisha muda wa viza cha asilimia 8.30, huku wale wa viza za F, M na J, zinazohusisha wanafunzi  na washiriki wa mipango ya  kubadilishana elimu, wakiwa na kiwango cha asilimia 13.97. Viza za B-1/B-2 hutolewa kwa safari za muda mfupi za kibiashara, utalii, mapumziko au matibabu. Viza za F, M na J hutolewa kwa wanafunzi wa kimataifa, watu wanaowategemea na washiriki wa mipango ya kubadilishana tamaduni na elimu, huku baadhi zikihitaji mhusika kurejea nchi anayotoka kwa angalau miaka miwili baada ya kumaliza masomo. Kwa hatua hii, Tanzania imejiunga na mataifa mengine yanayokabiliwa na vizuizi vya sehemu, yakiwemo Angola, Benin, Cote d’Ivoire, Gabon, Gambia, Malawi, Mauritania, Nigeria, Senegal, Zambia na Zimbabwe. Hatua hiyo inajiri kufuatia ripoti nyingi za ukiukaji wa haki za binadamu nchini Tanzania baada ya uchaguzi wa Oktoba. Awali, Amerika  ilikuwa imetishia kupitia upya uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Rais Samia Suluhu, ikitaka uwajibikaji kuhusu madai ya ukiukaji huo. Hata hivyo, serikali ya Rais Suluhu imepinga madai hayo, ikilaumu baadhi ya vyombo vya habari vya kikanda kwa kupotosha hali halisi na kichafua taswira ya Tanzania kimataifa. Wakati huo huo, Washington imeweka marufuku kamili ya kusafiri kwa raia wa Sudan Kusini, Syria, Burkina Faso, Mali na Niger, ikionyesha msimamo mkali zaidi kuhusu masuala ya uhamiaji. Rais Trump alisema uamuzi huo ulifikiwa baada ya kushauriana na maafisa wa baraza la mawaziri na kupitia ripoti ya awali chini ya Amri ya Rais 14161 na Tangazo 10949, pamoja na taarifa maalum za nchi zilizokusanywa baadaye.