RAIS wa Amerika Donald Trump amewasilisha kesi dhidi ya BBC akitaka alipwe Sh644 bilioni kwa kuhariri na kubadilisha hotuba yake ya Januari 6, 2021 kwenye taarifa ya uchunguzi zilizopeperushwa na kituo hicho cha habari. Trump amelaumu BBC kwa kumharibia jina na kukiuka kanuni za uanahabari akisema hivyo kwenye stakabadhi alizowasilisha kwa mahakama jijini Florida. Mwezi uliopita, BBC ilimwomba Trump msamaha lakini ikakataa amri yake ya kulipwa fidia ikisema hakukuwa na mahala popote ambapo jina lake lilichafuliwa. Mawakili wa Trump nao walishutumu BBC kwa kubadilisha hotuba yake wakiwa na nia ya kumwaibisha. Bado BBC haijajibu kesi iliyowasilishwa na Trump. Rais huyo alisema mwezi uliopita kuwa alikuwa amepanga kushtaki BBC kutokana na taarifa waliyopeperusha Uingereza kuelekea uchaguzi mkuu wa 2024 Amerika. “Nafikiri lazima niwashtaki. Walidanganya kwa sababu walibadilisha maneno kutoka kwa mdomo wangu,” akasema Trump. Katika hotuba yake Januari 6 2021, kabla ya maandamano Capitol, alionekana kuchochea mapigano. “Tutatembea Capitol na tutawashangilia maseneta wetu na wabunge wetu kwenye Bunge la Congress,” akasema wakati huo akilalamikia kuchezewa shere kwenye kura ya 2020. “Na tutapigana. Tutapigana kama ahera,” akaongeza. Kwenye taarifa zilizopeperushwa na BBC alinukuliwa vibaya na kuongezewa maneno. “Tutatembea Capitol na nitakuwa pamoja nanyi. Na tutapigana. Tutapigana kama ahera.” BBC ilikiri kuwa kuhariri hotuba hiyo kulileta picha mbaya kuwa Trump alikuwa akichochea maandamano lakini ikakanusha kuwa taarifa hiyo ilimharibia sifa. Mnamo Novemba, memo ya siri iliyofichuliwa kwa umma ilishutumu jinsi hotuba hiyo ilivyohaririwa na kubadilishwa na ikasababisha mkurugenzi mkuu wa BBC Tim Davie na mkuu wa habari Deborah Turnes wajiuzulu. Kabla ya Trump kuwasilisha kesi, mawakili wa BBC walikuwa wametoa majibu marefu kwa madai ya Trump. Walisema kuwa hakukuwa na kuchafuliwa jina na Trump hakuathirika au kuumizwa kwa sababu alichaguliwa tena baada ya taarifa hiyo kupeperushwa. Pia walisema BBC haikuwa na haki ya kusambaza habari hizo kwa vituo vyake Amerika kwa sababu taarifa hizo zilibanwa na kuonyeshwa kwa watazamaji wanaoishi Uingereza pekee. Viongozi mbalimbali Uingereza walimshutumu Trump kwa kuishtaki BBC. Waziri wa Afya Stephen Kinnock alisema BBC ilikuwa na haki ya kusimama kidete na kupambana na Trump mahakamani. “Naamini waliomba msamaha kwa makosa mawili matatu yaliyotokea. Pia wameweka wazi kuwa hakuna kesi ya kujibu kutokana na madai ya Trump kuwa alichafuliwa jina,” akasema Kinnock. Naye Sir Ed Davey ambaye ni Kiongozi wa Liberal Democrat alimtaka Waziri Mkuu Keir Starmer kumwambia Trump hatua yake ya kushtaki BBC haikubaliki kamwe. “Keir Starmer asimame na BBC dhidi ya matakwa yasiyofaa ya Trump la sivyo ni wanaolipia leseni ndio wataumia kifedha mahakama ikiamua alipwe,” akasema. Trump amewahi kushtaki vyombo kadhaa vya habari Amerika na kushinda baadhi ya kesi huku akitunukiwa mamilioni ya pesa.