WINGU jeusi la misukosuko ya kisiasa lilitanda mwaka mzima huku magavana watatu wakipitia makali ya mchakato wa kuwang’atua madarakani, hali iliyoangazia vita vya kisiasa kati ya magavana na wawakilishi wa wadi. Gavana wa Kericho Erick Mutai, mwenzake wa Isiolo Abdi Guyo na Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo waligonga vichwa vya habari baada ya migogoro yao na madiwani kuchochea azma ya kuondolewa kwao mamlakani. Mnamo Novemba 25, Gavana Nyaribo ambaye sasa anatajwa kama mfano wa gavana anayenusurika mara kwa mara hoja za kumwondoa ofisini zikiwasilishwa, alikabiliwa na jaribio la tatu la kung’atuliwa tangu achaguliwe tena mnamo 2022. Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja pia alinusurika njama ya kung’atuliwa mnamo Septemba baada ya Rais William Ruto na marehemu kiongozi wa ODM Raila Odinga kuingilia kati. Hali ilikuwa tete baada ya madiwani 87 kutia saini hoja ya kumng’atua Sakaja, hatua iliyomlazimu gavana huyo aliyetikiswa kisiasa kutafuta msaada wa aliyekuwa mbunge wa Westlands Fred Gumo na Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed, mshirika wa karibu wa Bw Odinga, ili kuokoa kiti chake. Gavana huyo wa muhula wa kwanza, aliyekuwa akilaumiwa kwa kutopatikana kwa urahisi, ghafla alipatikana na kuanza mikutano ya dharura huku akipigania uhai wake wa kisiasa. Baada ya vikao kadhaa, madiwani walishawishiwa kuachana na mpango huo, na kumuokoa Sakaja dhidi ya aibu ya kuwa gavana wa nne kuondolewa tangu uchaguzi wa 2022. Kwa magavana Mutai na Guyo, hoja zao za kuondolewa zilipitishwa katika mabunge ya kaunti lakini zikatupiliwa mbali na Seneti kwa misingi ya kukosa mashiko. Kwa Dkt Mutai, hii ilikuwa mara ya pili kunusuriwa na Seneti kwa msingi wa sababu za kung’atuliwa kwake kukosa mashiko, hali iliyoweka mabunge ya kaunti katika mizani kuhusu jinsi yanavyoendesha mchakato wa kung’atua magavana. Gavana Guyo naye alinufaika baada ya Seneti kuamua kuwa madiwani walishindwa kuthibitisha kuwa kikao halali kilifanyika, ikisisitiza kuwa mchakato wa kung’atua kiongozi ni muhimu sawa na matokeo ya kufanya hivyo. Majaribio haya yaliyofeli yamefichua uzembe katika baadhi ya hoja, huku wengine wakizitaja kama hujuma za kisiasa. Mapambano haya ya kisiasa, yanayochochewa zaidi na vita vya udhibiti wa mabilioni ya pesa za kaunti na siasa za urithi, yanatishia kuyageuza mabunge ya kaunti kuwa majukwaa ya “hoja za kung’atua zisizo na mwisho.” Tangu 2013, Seneti imeshughulikia zaidi ya kesi 20 za kuondoa magavana, ambapo ni nane pekee zilizothibitishwa. Kesi nyingi zilimhusu aliyekuwa Gavana wa Embu Martin Wambora, aliyenusurika mara nne na kupewa jina la “gavana mwenye maisha tisa,” jina ambalo sasa linaelekea kurithiwa na Gavana Mutai. Wakizungumza, maseneta na viongozi wa kitaifa wameonya dhidi ya matumizi mabaya ya hoja za kung’atua viongozi kama silaha za kisiasa badala ya zana za uwajibikaji. Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Ahmed Abdullahi alisema hoja nyingi za kuondoa magavana zinachochewa na siasa chafu, migawanyiko ya ndani na mipango ya urithi, badala ya ukiukaji halisi wa sheria. Spika wa Seneti Amason Kingi alisema atakutana na maspika wa mabunge ya kaunti ili kuweka miongozo itakayozuia hoja zisizo halali kufikishwa Seneti. Seneta wa Kakamega Boni Khalwale alipendekeza kutungwa kwa mwongozo rasmi wa kuwaelekeza madiwani, huku Seneta wa Narok Ledama Olekina akitaka Seneti izingatie hoja kwa misingi ya maudhui badala ya kiufundi.