Hofu ukame ukitanda kaunti kadhaa nchini

HALI ya ukame imetanda tena nchini na katika eneo lote la Afrika Mashariki, hali inayozua hofu sio tu ya njaa na vifo vya mifugo bali pia kurejea kwa migogoro inayochochewa na uhaba wa rasilmali. Kufeli kwa mvua za vuli za Oktoba hadi Desemba kumeacha jamii zinazotegemea maji na malisho zikijiandaa kwa miezi migumu ijayo, huku mamlaka zikikimbizana kuzuia ghasia ambazo kwa kawaida huambatana na vipindi virefu vya ukame. Kuanzia Pwani hadi maeneo kame ya kaskazini, dalili za hatari tayari zinaonekana. Katika Kaunti za Lamu na Kilifi, wakulima na wafugaji wanatazama anga kwa wasiwasi, wakifahamu kuwa kupungua kwa maji na malisho kunaweza kusababisha tena mivutano ya muda mrefu. Turkana na maeneo ya mipakani na Uganda, Ethiopia na Sudan Kusini, viongozi wanajitahidi kudumisha amani dhaifu huku wafugaji wakianza kuhama kutafuta malisho. Katika baadhi ya maeneo ya Lamu, tishio la ukame linafufua kumbukumbu za mapigano kati ya wafugaji na wakulima mifugo inapovamia mashamba. Bi Amina Ali, mkulima katika kijiji cha Kakathe, Witu, anasema migogoro kama hiyo imekuwa ya kawaida wakati wa kiangazi. “Malisho na maji yanapokauka, mifugo huingizwa mashambani na kuharibu mazao. Wakati mwingine watu huuawa, lakini udhibiti unaonekana kuwa mdogo,” alisema. Serikali za kaunti na kitaifa zinakiri hatari hiyo. Gavana wa Lamu, Issa Timamy, anasema kaunti imeweka njia za mifugo na kutenga maeneo ya malisho ili kupunguza migogoro, ingawa anakiri changamoto bado zipo. “Baadhi ya wakulima wamevamia njia za mifugo, huku baadhi ya wafugaji wakilisha mifugo mashambani. Haya yote yanazidisha hali tete,” alisema Bw Timamy, akiwaonya wafugaji dhidi ya kuvamia mashamba na wakulima dhidi ya kuziba njia za malisho. Kamishna wa kaunti, Wesley Koech, amesema vikosi vya usalama viko macho huku kiangazi kikizidi kushika kasi, akiwataka wakazi kutochukulia sheria mkononi. “Ukame si kisingizio cha kutoa vitisho, kuumiza au kuua wengine. Atakayevunja sheria atakamatwa,” alisema, akiongeza kuwa maeneo ya malisho yanatambuliwa kimataifa kama njia ya kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji. Viongozi wa wafugaji wanasema hatua za mapema ni muhimu. Bw Muhumed Kalmei, msemaji wa wafugaji Wasomali Lamu, aliwahimiza wafugaji kuondoka mashambani kwa hiari na akataka utekelezaji wa haraka wa maeneo ya malisho. “Tusisubiri hadi ukame ufikie hatua mbaya. Suluhisho lazima zitekelezwe sasa,” alisema. Wengine wanataka udhibiti mkali zaidi. Bw Abdurahman Abdi wa kijiji cha Mkunumbi alisema mifugo inayoingia Lamu kutoka Tana River na Garissa huongeza shinikizo za rasilmali na kuchochea mivutano. “Wafugaji wasio wa hapa wasajiliwe na machifu ili ijulikane ni nani na wanakusudia kukaa kwa muda gani,” alisema. Katika kilele cha ukame wa awali, Lamu ilipokea takriban mifugo 200,000 kutoka kaunti jirani. Shinikizo kama hilo linaonekana pia Magarini, Kilifi, ambako maelfu ya mifugo walivamia maji, kuchafua mabwawa na kuvuka maeneo yaliyotengwa, hali iliyosababisha vifo hapo awali. Kaunti za Kwale na Taita Taveta pia zimekumbwa na migogoro ya binadamu na wanyamapori wanapovamia mashamba kutafuta chakula na maji. Gavana wa Kwale, Fatuma Achani, amesema serikali yake inapanga kugawa chakula cha msaada kwa familia zilizoathiriwa. Kaskazini mwa Kenya, Turkana inaonyesha picha tofauti. Migogoro ya wizi wa mifugo na mapigano ya mpakani imepungua kufuatia juhudi za kudumisha amani na jamii za Uganda, Ethiopia na Sudan Kusini. Tamasha la Utalii na Utamaduni la Tobong’u Lore liliwakutanisha zaidi ya watu 30,000 kutoka jamii za Turkana, Samburu, Pokot na Ateker. Gavana wa Eastern Equatoria, Louis Lobong Lojore, alisema ushirikiano na Gavana Jeremiah Lomorukai umeimarisha ndoa za kijamii, matumizi ya pamoja ya rasilmali na huduma za msingi. Hata hivyo, Waziri wa EAC na Maendeleo ya Kikanda, Beatrice Askul, alionya kuwa ukame umekuwa ukisababisha migongano ya mpakani kutokana na ushindani wa maji na malisho. Mamlaka ya Ustawi wa Bonde la Kerio inaendelea kuchimba visima, kujenga mabwawa madogo na vidimbwi vya maji. Mkurugenzi wake Sammy Naporos alisema zaidi ya Sh200 milioni zimewekezwa katika miradi 17 inayohudumia watu 204,000 na mifugo 300,000.