NDUGU wawili na mchungaji wa mifugo ni miongoni mwa watu wanne waliofariki katika ajali ya barabarani iliyotokea Jumatano Desemba 17, 2025 usiku kwenye barabara kuu ya Namanga. Ajali hiyo iliyotokea mwendo wa saa tisa ilihusisha pikipiki na lori karibu na mahakama ya Kajiado. Mhudumu wa pikipiki na abiria wake watatu walifariki papo hapo. Waathiriwa waliokuwa wakitoka kwenye jumba la burudani walikuwa na umri wa kati ya miaka 40-47. Kulingana na ripoti ya polisi, lori hilo lililokuwa likielekea mji wa Kajiado lilikuwa likiendeshwa kwa kasi. Miili ya waathiriwa ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Rufaa ya Kajiado na mabaki ya lori na pikipiki kuvutwa hadi kituo cha Polisi cha Kajiado. Bw James Ole Sira, ambaye alipoteza jamaa yake katika ajali hiyo alisema, “Marehemu alikuwa mjomba wangu. Idadi ya vifo katika barabara kuu ya Namanga imeongezeka hivi karibuni," alisema Ole Sira. Katika muda wa wiki moja, jumla ya watu sita wamefariki katika ajali tofauti za barabarani katika barabara kuu ya Namanga, wengine wengi kujeruhiwa. Kamanda wa polisi kaunti ya Kajiado Alex Shikondi amewataka madereva wa magari kuepuka kuendesha magari kwakasi katika barabara kuu haswa nyakati za usiku.