KULIKUWA na kizaazaa Jumatano katika ofisi za utawala eneo la Mukuru-Hazina baada ya mvutano uliokuwa ukichemka kati ya maafisa wa polisi na wasimamizi wa serikali ya kitaifa kugeuka kuwa mzozo mkubwa, hali iliyoacha wakazi wengi wakiwa na mshangao na hofu. Mvutano huo ulifikia kilele pale maafisa wa polisi walipojenga ukuta wa mabati uliowazuia wasimamizi wa serikali kufikia Kituo cha awali cha Polisi cha South B, hatua iliyozua hasira miongoni mwa viongozi wa eneo hilo, wafanyabiashara na wakazi wa Mukuru-Hazina, eneo lenye idadi kubwa ya watu. Tofauti ya mihimili hiyo miwili ya serikali iliongezeka mapema asubuhi baada ya wasimamizi wa serikali kufika kazini na kukuta njia za kuingia kituo cha polisi zimefungwa. [caption id="attachment_182349" align="alignnone" width="2560"] Naibu Kamishena kaunti ndogo ya Starehe John Kisang akihutubia wananchi. Picha|Sammy Kimatu[/caption] Ukuta huo wa mabati ulijengwa kwa haraka usiku kucha, na kukatiza mawasiliano kati ya jengo la utawala na kituo cha polisi, ambavyo kwa miaka mingi vimekuwa vikishirikiana bila mipaka. Kwa mujibu wa mdokezi wetu, kisanga hicho kinahusishwa na uamuzi wa awali wa Kamanda wa Kituo cha Polisi cha South B (OCS), Bw Noor Mohammed, wa kuondoa miundombinu aliyodai kuwa ni haramu katika eneo la Hazina. Ubomoaji huo ulifanywa ili kupisha ujenzi wa kituo kipya cha kisasa cha polisi, mradi unaodaiwa kufadhiliwa kupitia Hazina ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF) na Mbunge wa Starehe, Bw Amos Mwago. Hatua hiyo haikuwafurahisha wasimamizi wa serikali za mitaa wala wafanyabiashara walioathiriwa na zoezi hilo. “Ubomoaji wa miundombinu hiyo haukuwapendeza wasimamizi na wafanyabiashara, jambo lililowasukuma machifu na wafanyabiashara kupinga,” mdokezi wetu aliarifu Taifa Leo . Hali ilizidi kuwa tata baada ya maafisa wa polisi kuondoa lango kuu la kuingia katika kituo cha zamani cha polisi na kulihamishia nyuma ya ofisi ya naibu chifu. Lango hilo liliripotiwa kupangiwa kutumika katika kituo kipya cha polisi kinachojengwa. [caption id="attachment_182348" align="alignnone" width="2560"] Wazee wa mtaa wakishangaa katika eneo la tukio. Picha|Sammy Kimatu[/caption] Wasimamizi wa serikali eneo la Hazina wanaongozwa na Msaidizi wa Kamishna wa Kaunti tarafa ya South B, Bw Ibrahim Adan, Chifu wa Hazina Bw Paul Muoki Mulinge na Naibu Chifu wa Hazina Bw Vincent Ambuga. Watatu hao walieleza wasiwasi wao kwamba hatua za polisi zilidhoofisha mamlaka yao na kuvuruga ushirikiano unaohitajika katika utoaji huduma kwa wananchi. Wakazi waliokusanyika eneo la tukio walihoji kwa nini taasisi mbili za serikali zilizopewa jukumu la kudumisha usalama na utulivu zilikuwa zikigombana hadharani. “Hivi sivyo tulivyotarajia. Ofisi hizi zinapaswa kufanya kazi pamoja kutulinda, si kupigana kama maadui,” alisema mkazi mmoja. Kamanda wa Kituo cha Polisi cha South B, Bw Noor Mohammed, aliyemrithi Bw Robert Mbui hivi karibuni, anajulikana kwa msimamo mkali dhidi ya uhalifu. Bw Noor aliwahi kusifiwa kwa kuongoza operesheni iliyobaini na kusambaratisha kiwanda haramu cha pombe ya chang’aa katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Reuben, Kaunti Ndogo ya Embakasi Kusini. Pia anatajwa kupunguza kwa kiasi kikubwa viwango vya uhalifu katika maeneo kadhaa hatari South B. [caption id="attachment_182350" align="alignnone" width="2560"] Msaidizi wa Kamishna tarafa ya South B, Bw Ibrahim Adan, Bw John Kisang (Naibu Kamishna kaunti ndogo ya Starehe), Chifu Paul Muoki Mulinge na naibuye, Bw Vincent Ambuga katika mzozo wa njia Mukuru-Hazina. Picha|Sammy Kimatu[/caption] Hata hivyo, mtazamo wake mkali unaonekana kuwakwaza baadhi ya viongozi wa eneo hilo, hasa baada ya agizo lake la kuondoa miundombinu haramu katika Hazina. Mvutano ulipozidi, wazee wa mtaa na wakazi wa Mukuru waliopinga maendeleo hayo walikusanyika karibu na ofisi za utawala wakitaka maelezo. Hali ilitishia kuharibika zaidi, na kuwalazimu wasimamizi wa serikali kutafuta uingiliaji wa mamlaka za juu. Hatimaye, Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Starehe (DCC) John Kisang, aliitwa kuingilia kati na kutuliza hali. Waandishi wa habari waliofika eneo la tukio walizuiwa kuripoti mkutano wa faragha uliofanyika baadaye katika ofisi ya Msaidizi wa Naibu Kamishna na kuongozwa na Bw Kisang. Mkutano huo uliwakutanisha wasimamizi wakuu wa serikali na wawakilishi wa polisi kwa lengo la kutuliza mzozo huo.