WANA wawili wa aliyekuwa mwanasheria mkuu nyakati za utawala wa hayati Daniel arap Moi , James Karugu wameshtakiwa kwa kumlaghai dada yao hisa katika kampuni ya uuzaji wa kahawa ya mabilioni ya pesa. Eric Mwaura Karugu na Benjamin Githara Karugu walishtakiwa pamoja na Jane Wangechi Kabiu almaarufu Jane Kabiu Gitau, ambaye ni Katibu wa kampuni hizo za Karugu aliyekuwa mwanasheria mkuu wa pili punde tu Kenya ilipojinyakulia uhuru. Watatu hao- Mwaura,Githara na Wangechi walikana mashtaka manne walipofikishwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Dolphina Alego. Watatu hao walikana shtaka la pamoja la kula njama kumlaghai Victoria Nyambura Karugu, bintiye mwanasheria huyo aliyeaga hisa. Walishtakiwa kwamba walihamisha hisa za Victoria kutoka Mathara Holdings Limited na kuziandikisha kwa kampuni ya Centurion Holdings Limited. Wangechi alishtakiwa peke yake kwa kuhamisha hisa hizo kwa njia ya ufisadi. Kiongozi wa mashtaka Hilary Isiaho alimshtaki Wangechi pia kwa kupelekea msajili wa kampuni fomu za kuhamisha hisa za Victoria kwa njia ya undanganyifu.. Mwaura na Githara walishtakiwa kwa kutoa habari za uwongo kwa afisa wa uchunguzi wa jinai (DCI) mnamo Feburuary 5,2025 kwamba walipewa fomu ya kuhamisha hisa za Victoria. Shtaka lilisema walimdanganya Peter Ouma kuhusu hisa hizo. Mahakama ilielezwa kutokana na habari hizo za kupotosha Insp Ouma alianza uchunguzi kubaini ukweli. Washtakiwa waliomba waachiliwe kwa dhamana wakisema ni haki yao ya kimsingi kwa mujibu wa katiba. Wakili mwenye tajriba ya juu Philip Murgor aliomba mahakama ihakikishe haki imetendeka kwa vile Victoria ameporwa hisa zake na sasa anataabika. Hakimu aliwaachilia kwa dhamana ya Sh1.5milioni na wadhamini wawili wa kiasi sawa na hicho. Pia walipewa dhamana ya Sh750,000 pesa tasilimu endapo hawatapata dhamana. Kesi hiyo itasikizwa Januari 20,2026. Jitihada za washtakiwa kupinga mashtaka yasisomwe ziligonga mwamba. Wiki iliyopita washtakiwa walikosa kufika kortini huku wakidai walikuwa sio buheri wa afya.