Maafisa watatu wa Sacco washtakiwa kwa wizi wa Sh40M

MAAFISA watatu wa chama cha ushirika cha wahudumu wa afya –Afya Sacco) wameshtakiwa kwa wizi wa Sh40milioni. Evans Mung’ahu Kola (meneja) alishtakiwa pamoja na Patrick Kuya Lubako na Mumina Mutinda Ing’ui kwa wizi wa Sh40,169,165.69. Watatu hao walikana mashtaka 11 walipofikishwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Lucas Onyina Desemba 19,2025. Kola, Lubako na Mutinda walikabiliwa na mashtaka ya kula njama za kulaghai Afya Sacco kwa kubuni akaunti feki za kuweka pesa na kuzitoa. Mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) alimweleza hakimu washtakiwa hao waliiba pesa hizo kutokana na nyadhifa zao kama wafanyakazi wa chama hicho cha ushirika. Pesa hizo hakimu alielezwa ziliibwa kati ya Aprili 20,2021 na Januari 3, 2025. Kola alikabiliwa na shtaka la kuiba Sh40,169,165.69 kutoka kwa Sacco hiyo. Nao Lubako na Mutinda walikana kuchomoka na Sh40,169,165.69 wakishirikiana na mtu mwingine ambaye hakufikishwa kortini. Lubako na Mutinda walikabiliwa na shtaka lingine la kujitajirisha na Sh10,714,999.72 wakijua zimepatikana kwa njia isiyo halali. Pia Lubako na Mutinda walikana walitia kibindoni Sh24,950,999.97 wakijua zimeibwa kutoka kwa akaunti ya Afya Sacco. Vile vile Kola na Mutinda walidaiwa kujinufaisha na Sh24,950,999.97 pesa za  Afya Sacco. Pia Kola na Mutinda walikana walijinufaisha na Sh1,702,000 zilizopatikana kwa njia isiyo halali pesa za Afya Sacco zilikuwa zimewekwa katika akaunti ya Fosa. Washtakiwa waliomba waachiliwe kwsa dhamana wakieleza korti walishirikiana na wachunguzi wa kesi hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja. Upande wa mashtaka haukupinga washtakiwa wakiachiliwa kwa dhamana. Mahakama iliombwa na DPP izingatie kiwango cha pesa kilichopotea ikiamua kiwango cha dhamana. Akitoa uamuzi  Bw Onyina alisema washtakiwa wamethibitisha kwamba hawatatoroka na watafika kortini wakati wa kusikizwa kwa kesi. Aliwaachilia kila mmoja na dhamana ya Sh4milioni na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho. Pia aliwapa dhamana badala ya Sh2milioni kila mmoja hadi Januari 6,2026 kesi itakatengewa siku ya kusikizwa.