ALIYEKUWA gavana wa Kiambu Ferdinard Waititu amepata ushindi mkubwa baada ya mahakama kunusuru baadhi ya mali zake zilizokuwa zimetwaliwa na serikali katika kesi iliyomkabili ya Sh1.9B. Mahakama iliamua kwamba Bw Waititu, ambaye kwa sasa yuko jela alieleza vya kutosha jinsi alivyopata mali na pesa katika akaunti za benki, ambazo zililengwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC). Waititu na mkewe Susan Wangari, hata hivyo, walipoteza mali kadhaa yakiwemo magari na ardhi ya thamani ya takriban Sh131 milioni, ambayo mahakama ilisema hakueleza vya kutosha jinsi alivyozipata. Gavana huyo wa zamani aliamriwa asalimishe magari mawili aina ya Toyota probox ya thamani ya Sh660,000, Toyota vitz ambayo thamani yake inakadiriwa kuwa Sh600,000, trakta yenye thamani ya Sh11 milioni na mashamba yake ya Thindigua, Kaunti ya Kiambu kila moja yenye thamani ya Sh32 milioni. Mkewe Susan aliagizwa kusalimisha sehemu ya ardhi ya Kitengela, kaunti ya Kajiado, yenye thamani ya Sh3 milioni. Kampuni inayohusishwa na gavana huyo wa zamani-Saika Two iliamriwa kusalimisha sehemu ya ardhi ijulikanayo kama Land House, yenye thamani ya Sh52 milioni. Kwa mali nyingine, mahakama ilisema maelezo yaliyotolewa na Waititu yalikuwa ya kuridhisha. 'Kuhusiana na fedha katika akaunti za benki, kama ilivyoelezwa katika hukumu kesi ya tume haikuwa nzuri au yenye msingi wala haki. Alichofanya mlalamishi (EACC) ni kuweka jumla ya pesa zilizokusanywa,' ilisema mahakama. Mahakama ilisema EACC ilipaswa kuweka salio katika akaunti za benki, kufanya uchanganuzi wa akaunti na kuonyesha ni pesa zipi zilishukiwa. Kwa mujibu wa mahakama, baadhi ya fedha hizo ni mikopo na za biashara ya kila siku pamoja na mauzo ya huduma na bidhaa. Gavana huyo wa zamani wa Kiambu alikuwa amezuiwa kuuza sehemu za ardhi 18 na magari hayo, kwani EACC ilisema yalinunuliwa kupitia ufisadi. Zaidi ya kuuza mali hiyo, wawili hao walizuiwa kukusanya kodi kutoka kwa Bienvenue Delta Hotel na mapato kutoka kwa Bins Management Services Ltd. Shirika la kupambana na ufisadi lilisema Waititu na mwenzake walipata mali hiyo kati ya 2015 na 2020 alipokuwa mbunge wa eneo bunge la Kabete na baadaye gavana wa Kiambu.