MAHAKAMA ya Ajira na Mahusiano ya Kazi imeidhinisha kufutwa kazi kwa mwalimu wa shule ya upili aliyeshtakiwa kwa kumnyanyasa kingono mwanafunzi wa kike kwa kumbusu na kumbatia. Katika uamuzi ulioweka misingi muhimu kuhusu uwajibikaji wa walimu na ulinzi wa wanafunzi katika mfumo wa elimu nchini, mahakama ilisema kuwa Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilifuata taratibu zote za kisheria na ilikuwa na sababu za kutosha za kumfuta kazi mwalimu huyo. Mahakama ilitupilia mbali ombi la aliyekuwa mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Muthurwa, aliyetambuliwa kwa herufi NP, aliyepinga kufutwa kwake kazi na kufutwa kwa usajili kama mwalimu akidai hatua hiyo ilikuwa kinyume cha Katiba na isiyo ya haki. NP alidai kuwa waliomshutumu hawakutoa ushahidi dhidi yake wakati wa vikao vya nidhamu na kwamba alinyimwa nafasi ya kuwauliza maswali mashahidi. Aliomba mahakama iamue kuwa TSC ilikiuka haki yake ya usimamizi wa haki wa kiutawala, pamoja na kurejeshwa kazini na kulipwa fidia. Hata hivyo, mahakama iliamua kuwa ushahidi uliowasilishwa dhidi yake ulikuwa wa kuaminika na kwamba taratibu zote zilifuatwa ipasavyo. “Ushahidi uliotolewa ulionyesha wazi hatia ya mlalamishi kwa mashtaka yaliyomkabili,” mahakama ilisema. “Kulikuwa na sababu halali za kumfuta kazi, na haki ya mchakato iliheshimiwa.” Jaji alitaja madai ya kukiukwa kwa haki yake “yasiyo na msingi” na kuthibitisha kuwa NP “alifutwa kazi kwa haki na kwa misingi halali.” Kesi hiyo ilitokana na madai ya Septemba 2023 kwamba NP alimwita mwanafunzi wa kidato cha nne kutoka darasani wakati umeme ulipokatika na kumbusu kwenye ngazi za shule. Mashahidi pia walidai kuwa alimkumbatia kwa nguvu, akamgusa matiti bila idhini, na kufanya vitendo visivyofaa wakati wa kipindi cha kusoma darasani. Katika vikao vya nidhamu mbele ya Bodi ya Usimamizi wa Shule (BOM) mnamo Oktoba 2023, NP alikabiliwa na mashtaka ya kudumisha uhusiano haramu na mwanafunzi huyo, kinyume na sera za TSC, na pia kukiuka kanuni za shule kwa kumpa simu yake ya mkono. Ushahidi wa video ulionyeshwa akimkumbatia na kumbusu mwanafunzi huyo, kumshika kiunoni kwa nguvu na kumgusa titi, licha ya mwangaza hafifu. Mahakama iliamua kuwa TSC ilianzisha hatua za kinidhamu kwa mujibu wa Kanuni za Maadili kwa Walimu, ikimpa NP barua ya kujieleza kabla ya kumfikisha mbele ya BOM. Mwanafunzi na mashahidi wengine walitoa ushahidi mbele yake, na alipewa fursa ya kuwauliza maswali. “Mwathiriwa alitoa ushahidi dhidi yake na alitumia haki yake ya kuhoji maelezo yake,” mahakama ilisema, ikikataa madai ya kutumiwa kwa ushahidi wa kusikia tu au ukiukaji wa taratibu. Baada ya uamuzi wa BOM, NP alisimamishwa kazi na baadaye akafikishwa mbele ya kamati ya nidhamu ya TSC, ambapo mwanafunzi huyo alirudia madai yake. Wanafunzi wenzake walithibitisha ushahidi huo wakisema walimuona mwalimu huyo akiwa na mwanafunzi na kusikia kelele karibu na ngazi. Mahakama ilisema ushahidi huo ulikuwa thabiti katika vikao vyote viwili, huku NP akihudhuria na kupewa nafasi ya kuwauliza mashahidi maswali kila mara. Katika ombi lake, NP alidai madai hayo yalitungwa, yalicheleweshwa na hayakuwa na ushahidi wa kitabibu au wa kimwili. Pia alishutumu TSC kwa kubadilisha barua ya kusimamishwa kazi na kukiuka haki zake za kikatiba za utu, haki ya kiutawala na ajira ya haki. Mahakama ilitupilia mbali hoja hizo, ikisema kuwa vikao vya kinidhamu si kesi za jinai na vinahitaji tu kuthibitishwa kwa utovu wa nidhamu, si viwango vya ushahidi vya mahakama ya jinai. “TSC ilifikia uamuzi wa busara kwamba kulikuwa na utovu wa nidhamu kulingana na ushahidi wa mashahidi,” jaji alisema. “Hakukuwa na ukiukaji wa haki za kikatiba kwani mchakato ulikuwa wa haki na wenye msingi.” TSC ilitetea hatua zake kama muhimu kulinda wanafunzi na kudumisha viwango vya taaluma ya ualimu, ikirejelea ulinzi wa kikatiba dhidi ya unyanyasaji wa kingono shuleni. Mahakama ilikubaliana na msimamo huo, ikisisitiza kuwa madai yanayohatarisha ustawi wa wanafunzi yanapaswa kushughulikiwa kwa uzito. Jaji alikataa kurejeshwa kazini au kulipwa fidia, akisema itakuwa kinyume na maslahi ya umma kumrejesha mwalimu aliyefutwa kazi kwa kosa la unyanyasaji wa kingono. NP, aliyeajiriwa mwaka 2019 kama mwalimu wa shule ya upili, alipoteza kesi yake yote, huku kila upande ukibeba gharama zake.