TAWE! Sababu ya miswada minane ya sheria aliyotia saini Ruto 2025 kupingwa vikali

ASUBUHI ya Oktoba 15, wakati Wakenya walikuwa bado wanakabiliana na habari za kifo cha kinara wa upinzani Raila Odinga aliyefariki dunia akiwa India, Rais William Ruto alitia saini miswada minane kuwa sheria katika Ikulu ya Nairobi. Sheria hizo zilizotiwa saini siku hiyo ya maombolezo kwa taifa zilijumuisha Sheria ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Uhalifu wa Mtandaoni (Marekebisho), Sheria ya Uhifadhi na Usimamizi wa Wanyamapori (Marekebisho) na Sheria ya Tume ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi (Marekebisho). Nyingine ni Sheria ya Ardhi (Marekebisho), Sheria ya Tume ya Kitaifa ya Ardhi (Marekebisho), Sheria ya Ada ya Huduma kwa Abiria wa Anga (Marekebisho), na Sheria ya Ubinafsishaji. Aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga alikuwa miongoni mwa viongozi mashuhuri waliomkosoa Rais Ruto kwa hatua hiyo ya kutia saini miswada minane siku hiyo. Jaji Maraga aliishtumu serikali kwa jaribio la “kuwaibia Wakenya” kwa kumpa Rais na Waziri wa Fedha mamlaka makubwa yasiyodhibitiwa ya kuuza mali ya taifa. Mswada huu ulibadilisha Sheria ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Uhalifu wa Mtandaoni, Sura 79C, ili kuimarisha vipengele vinavyokataza matumizi ya majukwaa ya kielektroniki kuendeleza shughuli haramu, ponografia ya watoto, ugaidi, misimamo mikali ya kidini na ibada za kishetani, unyanyasaji mtandaoni na ulaghai. Marekebisho hayo yalipatia Kamati ya Kitaifa ya Uratibu wa Masuala ya Kompyuta na Uhalifu wa Mtandaoni mamlaka ya kutoa maagizo ya kuzima au kuzuia tovuti au apu endapo itathibitika kuwa zinakuza shughuli haramu, ponografia ya watoto, ugaidi au misimamo mikali ya kidini. Sheria pia ilirekebisha Kifungu cha 27 ili kupanua kosa la unyanyasaji mtandaoni, likijumuisha visa ambapo mhusika anajua kuwa matendo yake yanaweza kumshawishi mtu kujiua. Hata hivyo, wanasheria wameonyesha wasiwasi kuwa sheria hiyo inaweza kusababisha uhalalishaji wa kiholela wa mjadala halali wa umma kuhusu masuala muhimu ya kitaifa. Pia kuna hofu kuhusu Kifungu cha 27 kinachoharamisha kauli zinazodaiwa kumdhuru mtu ikiwa ni chafu au zinakera sana, au zinazoweza kusababisha hofu, kwa kuwa haijabainishwa wazi ni nani ataamua nini ni “kinachokera sana”. Sheria ilirekebisha Sheria ya Uhifadhi na Usimamizi wa Wanyamapori, Sura 376, ili kujumuisha wanyama wa baharini miongoni mwa wale ambao waathiriwa wanaweza kulipwa fidia kwa majeraha au vifo. Hata hivyo, sheria hiyo imeibua pingamizi huku Bunge likituhumiwa kutenga jamii zilizotengwa ambazo zinaathirika zaidi na utekelezaji wake. Mashirika ya kijamii yakiwemo Ulinzi Africa, Pwani Animal Welfare, Muslims for Human Rights na Care Animal Welfare yalisema kuwa ushirikishaji wa umma haukuwa wa kutosha na mchakato uliharakishwa. Sheria ya Ardhi (Marekebisho), 2022 inamlazimisha Msajili Mkuu wa Ardhi kusajili ardhi yote ya umma iliyotolewa kwa taasisi za umma na Tume ya Kitaifa ya Ardhi, pamoja na ardhi iliyotengwa na waendelezaji kwa matumizi ya umma kama ilivyoainishwa katika mipango ya maendeleo iliyoidhinishwa. Hata hivyo, kuna wasiwasi kuwa sheria hiyo inaweza kudhoofisha mamlaka ya Tume ya Kitaifa ya Ardhi kwa kuweka muda wa miaka mitano pekee wa kushughulikia migogoro ya ardhi na mapitio ya umiliki wa kihistoria. Sheria ya Ubinafsishaji, 2025 inaweka utaratibu wa kuidhinisha uuzaji wa mali na hisa za serikali kupitia Baraza la Mawaziri na Bunge la Kitaifa. Hata hivyo, sheria hiyo imepingwa mahakamani kwa madai kuwa ilitungwa bila ushirikishaji wa umma wa kutosha, kinyume na Katiba. Walalamishi wameonya kuwa kuweka miundombinu muhimu ya taifa mikononi mwa sekta binafsi kunaweza kuhatarisha maslahi ya umma, kwa kuwa lengo kuu la wawekezaji wa kibinafsi ni faida, si ustawi wa wananchi.