Wito wazazi waimarishe ulinzi wa watoto wao wakati wa Krismasi

SHEREHE za sikukuu zinapoanza, Naibu Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kaunti ya Nairobi, Waithera Chege, amewataka wazazi na walezi kuweka mbele usalama na ustawi wa watoto wao. Bi Chege amesema kuwa kipindi cha sikukuu huongeza hatari kwa watoto zikiwemo ushawishi mbaya wa marafiki, kuwindwa na wahalifu wa kingono, pamoja na matumizi ya dawa za kulevya na pombe. Kwa mujibu wake, vitendo hivyo huongezeka wakati wa likizo, hivyo wazazi wanapaswa kuwa macho na kuchukua hatua za mapema kuwalinda watoto. Akizungumza wakati wa hafla ya kutoa msaada katika Wadi ya Nairobi South, ambapo aligawa vyakula, magodoro, blanketi na pesa taslimu kwa wakazi—wengi wao wakiwa waathiriwa wa moto ulioteketeza makazi katika eneo la Fuata Nyayo, Bi Chege alisisitiza umuhimu wa wazazi kushirikiana katika kulinda watoto. “Ulinzi wa watoto si jukumu la mzazi peke yake. Jamii nzima, viongozi wa mitaa na vyombo vya usalama vinapaswa kushirikiana ili kuhakikisha mazingira salama,” alisema. Diwani huyo wa Nairobi South pia alitoa wito kwa vyombo vya usalama kuongeza doria na kuimarisha ulinzi katika eneo la South B wakati wa sikukuu, ili familia ziweze kusherehekea Krismasi kwa amani na usalama. Aliwahimiza wazazi kufuatilia mienendo ya watoto wao, kujenga mawasiliano ya karibu, na kushirikiana na majirani kuripoti vitendo vinavyohatarisha usalama wa watoto, akisisitiza kuwa ulinzi wa mtoto ni msingi wa mustakabali wa jamii.