Dar es Salaam. Kufuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 uliofaa sintofahamu, chama cha ACT-Wazalendo kimefungua jumla ya kesi 83 hadi sasa kupinga matokeo yaliyowapa ushindi wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika kata/wadi na majimbo mbalimbali Bara na Zanzibar, likiwemo jimbo la Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ni Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani, Pemba, ambaye miongoni mwa majukumu yake ni kumsaidia Rais wa Zanzibar katika utekelezaji wa sera za Serikali, uendeshaji wa shughuli za Bunge la Wawakilishi na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kutokana na matokeo ya uchaguzi huo, chama hicho kimefungua jumla ya kesi 83 nchini kote, Bara na Zanzibar, zinazojumuisha kesi za udiwani na ubunge kwa Bara, uwakilishi na ubunge kwa Zanzibar. Kesi hizo zimefunguliwa na wanachama wa ACT-Wazalendo, wengi wao walioshiriki katika uchaguzi huo na kuwa wagombea wa nafasi mbalimbali. Katika jimbo moja, kesi hiyo ilifunguliwa na wapiga kura, waliokuwa na lengo la kutilia shaka matokeo ya uchaguzi na kuhakikisha haki zao za kidemokrasia zinatimizwa. Wamefungua kesi hizo dhidi ya mamlaka za usimamizi na uendeshaji uchaguzi, yaani Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa Tanzania na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) pamoja na wasimamizi wa uchaguzi na washauri wa Serikali wa masuala ya kisheria, yaani Wanasheria Wakuu wa Serikali. Katika kesi hizo chama hicho kinapinga matokeo hayo kikidai uchaguzi huo uligubikwa na kasoro nyingi, zikiwemo ukiukwaji wa taratibu, kanuni na sheria za uchaguzi na mambo mengine yasiyostahili kufanyika wakati wa uchaguzi wa kidemokrasia. Kesi hizo ambazo ni hatua ya chama hicho kubadili matokeo hayo kwa njia za kisheria, ziko katika hatua mbalimbali kuelekea usikilizwaji wa madai ya msingi ya walalamikaji, yaani usikilizwaji wa ushahidi na utetezi ambao mahakama itautumia kuupima katika uamuzi wake. Mchanganuo wa kesi Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama hicho pamoja na maelezo ya ufafanuzi kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa ACT-Wazalendo, Omary Said Shaaban, kwa Zanzibar chama hicho kimefungua jumla ya kesi 59 zilizofunguliwa Pemba na Unguja. Kwa upande wa Pemba chama hicho kimefungua kesi 23, kesi moja ya udiwani, nane za uwakilishi na 14 za ubunge, Mahakama Kuu ya Zanzibar, Kanda ya Pemba. Majimbo ambayo matokeo ya uwakilishi yanapingwa ni pamoja na Kiwani, ambako Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla alitangazwa mshindi; Mkoani, Chakechake, Chonga, Wawi, Kojani, Konde na Micheweni. Kesi hizo zitatajwa tena mahakamani hapo Desemba 23 kwa ajili ya kuangalia kama taratibu za ubadilishanaji nyaraka umekamilika, kisha majalada yapelekwe kwa Jaji Mkuu kwa ajili ya kupangiwa majaji wa kuzisikiliza. Kwa upande wa kesi za ubunge, majimbo ambayo matokeo yake yanapingwa Pemba ni Wete, Gando, Kojani, Micheweni, Konde, Wingwi, Ole, Ziwani, Wawi, Chake Chake, Chonga, Kiwani, Chambani na Mkoani. Kwa upande wa Unguja zimefunguliwa jumla ya kesi 36 katika Mahakama Kuu Tunguu, kati ya hizo, za uwakili 17 na za ubunge 19. Majimbo ambayo matokeo ya uwakilishi yanapingwa ni Nungwi, Kijini, Mkwajuni, Chaani, Tumbatu, Bimbwini, Mtoni, Mwera, Welezo Pangawe, Mwanakwerekwe, Chumbuni, Mpendae, Amani, Malindi, Kiembesamaki na Makunduchi. Kwenye kesi hizo hatua za usikilizwaji wa awali yaani ubadilishanaji nyaraka za kesi baina ya pande mbili husika zimeshakamilika na sasa zinasubiri kupangiwa majaji kwa ajili ya kuanza uaikilizwaji kamili. Kwa upande wa ubunge, majimbo ya Unguja ambayo matokeo yake yanapingwa ni Nungwi, Kijini, Mkwajuni, Chaani, Tumbatu, Bimbwini, Mtoni, Mwera, Welezo, Pangawe, Mwanakwerekwe, Chumbuni, Mpendae, Amani, Malindi, Kiembesamaki, Makunduchi, Dimani na Shaurimoyo. Kesi hizo ziko katika hatua za mwisho za maandalizi ya usikilizwaji kamili ambapo walalamikaji watawasilisha ushahidi kuthibitisha madai yao kabla ya walalamikiwa kujibu na hatimaye mahakama kuandaa na kutoa hukumu. Kesi zilizofunguliwa Bara Kwa upande wa Tanzania Bara, chama cha ACT-Wazalendo kimefungua jumla ya kesi 24 katika mikoa na mahakama tofautitofauti, za udiwani na ubunge. Kati ya hizo kesi za udiwani ni 19 na za ubunge ni tano. Matokeo ya udiwani yanayopingwa ni katika kata za Roche-Rorya, iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, Mara; Kata ya Mzimuni-Kinondoni, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni inayoketi Kinondoni Dar es Salaam. Nyingine ni Kata za Kunduchi, Hananasifu, Temeke, Mianzini, Kilakala, Miburani, Mtoni Sandali, Keko, Ubungo, Kurasini, Bunju, Manzese, Kipugira na Mabibo, zilizofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu. Pia, kuna Kata ya Kyaka mkoani Kagera iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba; Kata ya Kerenge, mkoani Tanga iliyofunguliwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga. Kwa upande wa kesi za ubunge majimbo ambayo matokeo yake yanapingwa ni pamoja Jimbo la llala, la Spika wa Bunge, Mussa Hassan Zungu iliyopo Mahakama Kuu Dar es Salaam na Jimbo la Lindi Mjini, mkoani Lindi, Mahakama Kuu Ndogo Mtwara. Pia, Jimbo la Tunduru Kusini iliyopo Mahakama Kuu Songea, Jimbo la Rungwe mkoani Mbeya, Mahakama Kuu Mbeya na jimbo la Kigoma Mjini, Mahakama Kuu Kigoma. Wakati katika kata na majimbo mengine kesi hizo zikiwa zimefunguliwa na waliokuwa wagombea, katika jimbo la Kigoma Mjini kesi hiyo imefunguliwa na wapiga kura wanne. Wapiga kura hao ni Johary Kabourou, Loum, Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali, dhidi ya Tume Huru ya Uchaguzi, mbunge wa jimbo hilo, Clayton Revocatus Chipando maarufu kama Baba Levo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Katika uchaguzi Chipando, alitangazwa kuwa mshindi dhidi ya mpinzani wake mkubwa kutoka Chama cha ACT-Wazalendo, mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Zitto Kabwe. Katika kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya mwaka 2025 inayosikilizwa na Jaji Projestus Kahyoza iko katika hatua za mwisho kuelekea usikilizwaji kamili.