Serikali ya Nyong’o yajitetea kwa kutotumia senti kufanya miradi

SERIKALI ya Kaunti ya Kisumu chini ya Gavana Profesa Anyang’ Nyong’o, imejitokeza kufafanua sababu ya kutotumia hata shilingi moja kwenye miradi ya maendeleo katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26, ikikiri kuwa fedha hizo zilitumika kushughulikia dharura nyingine ya kifedha. Kulingana na ripoti ya Mdhibiti wa Bajeti, Kaunti ya Kisumu ilikuwa miongoni mwa kaunti 20 ambazo hazikutumia pesa zozote katika maendeleo kati ya Julai na Septemba 2025. Ripoti hiyo ilionyesha picha ya kusikitisha ya miradi iliyokwama katika kaunti nyingi, huku matumizi makubwa yakielekezwa kwa gharama za kawaida, hali iliyozua maswali kuhusu vipaumbele vya serikali za kaunti chini ya mfumo wa ugatuzi. Hata hivyo, kupitia Waziri wa Fedha wa Kaunti, George Okong’o, serikali ya kaunti ilieleza kuwa Sh128.4 milioni zilizotengwa kwa maendeleo zilitumika kulipa mishahara ya wafanyakazi wa Hospitali ya Rufaa ya Mafunzo na Utafiti ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOTRH). Bw Okong’o alisema kuwa baada ya hospitali hiyo kugeuzwa kuwa shirika la umma, kulizuka pengo la kifedha katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha, jambo lililolazimu kaunti kuingilia kati. Alieleza kuwa kwa ombi la Serikali ya Kitaifa na kwa misingi ya ushirikiano wa kiserikali, Kaunti ya Kisumu ilitoa fedha hizo kama mkopo wa muda ili kuhakikisha mishahara ya wafanyakazi wa hospitali inalipwa kwa wakati, wizara ya fedha ikiendelea kukamilisha taratibu za kuhamisha fedha husika. “Jumla ya Sh128,482,567.55 ambazo awali zilitengwa kwa maendeleo katika robo ya kwanza, zilitolewa kama mkopo kulipa mishahara ya wafanyakazi wa JOOTRH. Hii ndiyo sababu hakuna matumizi ya pesa kwa maendeleo yaliyoonekana katika kipindi hicho,” alisema Bw Okong’o.Alisisitiza kuwa fedha hizo hazikupotea, kuibwa wala kutumiwa vibaya, akieleza kuwa JOOTRH tayari imepokea mgao wake kutoka Wizara ya Fedha na mchakato wa kurejesha fedha hizo kwa kaunti unaendelea. Aliahidi kuwa fedha zitakaporejeshwa, zitaelekezwa kikamilifu kwa miradi ya maendeleo.