MKUTANO wa Rais William Ruto na kundi la wabunge kutoka kaunti za Kisii na Nyamira uliofanyika Ijumaa, Desemba 19, 2025, Ikuluni, ulitafsiriwa hadharani kama kikao cha kawaida cha maendeleo, lakini kwa undani uliashiria mabadiliko makubwa ya kisiasa yanayoendelea katika eneo hilo. Haya yanajiri huku aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, akiibuka kama nguzo muhimu katika upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. Kikao hicho cha faragha kilichodumu takribani saa mbili kiliwaleta pamoja wabunge wanaounga mkono chama tawala cha UDA pamoja na baadhi ya wanasiasa wa upinzani ambao hivi majuzi walianza kuunga mkono serikali jumuishi ya Rais Ruto na chama cha ODM. Ingawa waliohudhuria walisisitiza kuwa ajenda kuu ilikuwa maendeleo, muda na muundo wa ujumbe ulionyesha malengo ya kisiasa ya kurejesha ushawishi uliopotea katika chaguzi ndogo za hivi karibuni na kudhibiti mvuto unaoongezeka wa Dkt Matiang’i. Mkutano huo ulifanyika wiki chache baada ya wagombeaji wanaohusishwa na Matiang’i na chama cha Jubilee kushinda chaguzi ndogo za wadi Nyamira, jambo lililokuwa pigo kwa viongozi wanaoegemea UDA na kuzua maswali kuhusu umaarufu wa chama tawala katika eneo hilo. Mbunge wa South Mugirango ambaye ni kiranja wa wengi katika Bunge la Kitaifa, Silvanus Osoro, aliyekuwa kiongozi wa ujumbe huo, alipuuza madai kuwa jina la Matiang’i lilijadiliwa Ikulu. Alisema mazungumzo yalihusu maandalizi ya ziara ya maendeleo ya Rais katika eneo la Gusii, ambako miradi kadhaa inatarajiwa kuzinduliwa. Hata hivyo, kauli za baadhi ya wabunge zilionyeesha hofu ya kisiasa. Mbunge wa Nyaribari Chache, Zaheer Jhanda, alimkosoa Matiang’i akisema hana muundo thabiti wa kisiasa na juhudi zake si za kitaifa. Ajenda ya maendeleo ilijumuisha kituo cha matibabu ya saratani cha Sh4.7 bilioni kinachofadhiliwa kwa pamoja na Kenya na Saudi Arabia pamoja na miradi ya barabara katika Kisii na Nyamira. Viongozi wa UDA wanategemea miradi hiyo kama ushahidi wa uwepo wa serikali mashinani. Kwa upande wake, Seneta wa Kisii Richard Onyonka alisema hali halisi mashinani inaonyesha kuwa wakazi wengi tayari wamejipanga kumuunga mkono Dkt Matiang’i kutokana na kuchoshwa na ahadi zisizotekelezwa, gharama ya juu ya maisha na siasa za kimaslahi..