Polisi wa ‘Ruto Must Go’ ashindwa kuokoa kazi yake kortini

AFISA wa polisi aliyekuwa kwenye video ya Tiktok yenye kauli-mbiu ‘Ruto Must Go’ (Sharti Ruto Ang’atuke), amepoteza kesi aliyowasilisha mahakamani kuzuia Tume ya Huduma za Polisi (NPSC) kumwachisha kazi. Mahakama ya Leba ilitupilia mbali kesi ya Joyfred Maina ikisema alikuwa amewasilisha kesi hiyo huku rufaa yake aliyokata kwa tume ya NPSC ikiwa bado inaendelea. Bw Maina ambaye awali alihudumu katika Kituo cha Polisi cha Riruta alikuwa amepinga kutimuliwa kwake mnamo Septemba 2024 kutokana na video hiyo ambayo ilizua maoni kinzani, ikishabikiwa na na kukosolewa na Wakenya kwa wakati mmoja. Mahakama iliamua kuwa afisa huyo aliwasilisha kesi ilhali pia alikuwa ameiwasilisha rufaa kwa idara za NPSC zinazohusika na kufutwa. Kwa hivyo, ni vyema angesubiri matokeo ya uamuzi wa rufaa aliyowasilisha kabla ya kukimbia kortini. “Hakuna pingamizi kwamba amefuata mkondo wa kupata haki kupitia vyombo vya ndani katika idara ya polisi. Mahakama haiwezi kutoa uamuzi kabla ya rufaa yake kuamuliwa,” ikasema mahakama. Kesi hiyo ilitokana na yaliyotokea wakati wa maandamano ya kitaifa dhidi ya serikali mnamo Julai 19, 2023. Kulikuwa na uhasama mkali wa kisiasa kati ya upinzani na serikali wakati huo baada ya uchaguzi wa 2022. Bw Maina alikuwa Polisi wa Utawala (AP) aliyejiunga na idara hiyo kama mlinzi wa kituo mnamo 2008. Alishiriki video hiyo akiwa amevaa sare katika hali ambayo inadhaniwa kuchangia kuibuka kwa kauli ‘Ruto Must Go’ miongoni mwa wakosoaji wa Rais. Bw Maina alijitetea tu akisema alisoma kwa sauti yale yaliyoandikwa kisha akawaonya watazamaji dhidi ya kutumia lugha kama hiyo. Mahakama iliambiwa kuwa video hiyo ilisambaa kwa kasi baada ya kuhaririwa na watu wasiojulikana na kuchochea ghadhabu za umma. Pia ilisababisha mienendo ya polisi ichunguzwe wakati wa maandamano. Makamanda wa polisi walisema video hiyo ilikuwa kinyume cha utendakazi wa idara hiyo na kuonyesha walikuwa wakiegemea upande mmoja kisiasa. Siku iliyofuatia, Bw Maina alitumiwa notisi ya kumtaka aeleze kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu. Alitakiwa kujitetea kwa makosa ya kutoa matamshi ya uchochezi, uongo, kutelekeza majukumu yake na kukiuka kanuni za utendakazi wa idara ya polisi. Baada ya kujibu notisi hiyo, Bw Maina alifutwa kazi ila baadaye akasimamishwa na kesi yake kufuata mkondo wa maamuzi ya ndani kwenye NPS. Kamati ya nidhamu ilibaini kuwa haina mamlaka ya kutosha ya kusikiliza rufaa ya Bw Maina hivyo basi ikaiwasilisha kwa makamanda wao wakuu. Mnamo Septemba 2024, NPSC ilimwondoa rasmi na kusema adhabu hiyo ilistahili kuanza siku aliyosimamishwa. Alishauriwa akate rufaa ndani ya siku 14. “Kufuatia uzito wa utovu wa nidhamu na rekodi yake ikiwemo kutelekeza majukumu, kamati inapendekeza afutwe kazi,” akasema Silas Andiema, Kamishina wa Polisi anayehusika na Masuala ya Wafanyakazi kwenye stakabadhi za korti. Bw Maina akiwa mbele ya mahakama alisema kuwa haki zake za kikatiba zilikuwa zimekiukwa akitaja kanuni za leba zinazostahili kuzingatiwa na kusikizwa kwake. Alidai kuwa mchakato wa nidhamu ulikuwa umevurugika na hakupewa notisi ndani ya siku saba kabla ya kupitishwa kwenye mkondo wa nidhamu. Alidai kuwa haki ya kujieleza pia ilikiukwa kinyume cha sheria, akisema kuwa hafai kuzuiwa kuzungumza au kutangamana na umma kwa sababu yeye ni afisa wa polisi. “Sikupewa nafasi ya kuwasilisha kesi yangu au kusikizwa wakati wa rufaa,” Bw Maina akaambia mahakama akiomba arejeshwe kazini, kufutiliwa mbali kwa kutimuliwa kwake na alipwe kwa muda ambao hajakuwa kazini. Hata hivyo, Inspekta Jenerali wa Polisi na Mwanasheria Mkuu walipinga kesi hiyo wakisema alitumuliwa kwa haki na sheria kufuatwa. Mawakili walisema kuwa tabia ya afisa huyo akiwa amevalia sare ilikiuka hitaji la kisheria kuwa maafisa wa usalama hawafai kuwa na miegemeo ya kisiasa.