Kinaya kisiwa cha Mombasa kukosa fukwe za kuvinjari

WAKAZI na wadau wa utalii kisiwani Mombasa wametoa wito fukwe zilizo ndani ya kisiwa zifanyiwe ukarabati. Fukwe za ndani ya kisiwa, kama Madhubaha, ufuo wa Fort Jesus na Tudor, zimetelekezwa, hali inayolazimu wakazi kutegemea zile zilizo kaskazini mwa Mombasa kama vile Bamburi na Nyali. Eneo pekee la umma la mapumziko ufukweni linalosifika ni bustani ya Mama Ngina, ambayo ilifunguliwa upya Oktoba 20, 2019 na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, baada ya ukarabati uliogharimu karibu Sh460 milioni. Awali, eneo hilo pia lilitelekezwa na kulifanya kuwa maficho ya wahalifu. Imebainika kuwa, fukwe zilizotelekezwa za kisiwa hicho huwa chafu kwa sababu maji ya mvua yanayobeba uchafu huelekezwa huko, mbali na majitaka. Bw Ahmed Said Mbarak, kutoka Fort Jesus, anaamini eneo hilo likifanyiwa ukarabati linaweza kuleta manufaa makubwa hasa kwa sekta ya utalii. “Eneo hili lina uwezo mkubwa kwa sababu Fort Jesus huvutia watu wengi. Kama tungekuwa na eneo zuri la mapumziko, mambo yangekuwa tofauti. Kwa sasa ni miamba na maji ya mvua tu; kubadilisha hali hii kutahitaji juhudi kubwa,” akasema. Zamani, vijana walikusanyika hapo kwa ajili ya kupiga mbizi na kuogelea, hasa wikendi. “Siku hizi watu huja tu kuona mandhari kisha huondoka. Wakazi wameunganisha mabomba yao ya majitaka kwenye mifereji ya maji ya mvua, hali inayowafanya watu kuchukia kuogelea hapa,” anaongeza. Kwa sasa, ni wakazi wachache tu wanaoweza kustahimili maji machafu na kuingia baharini kuogelea. Katika eneo la Tudor, kuna ufuo mwingine ambao ungestahili kuwa na shughuli nyingi. Kama ilivyo katika maeneo mengine ya kisiwa, harufu ya majitaka yanayoingia baharini hapa huwafukuza watu isipokuwa wale wenye ujasiri wa kuingia kwenye maji hayo. Bw Abdalla Mangale, mlinzi wa kujitolea wa baharini katika Tudor Beach tangu mwaka wa 2020, anasema kuwa licha ya juhudi zake za kusafisha na kupamba eneo hilo, huvutia watu wachache. “Niliamua kubaki hapa kwa ajili ya watoto wanaokuja kuogelea; hapo awali ajali zilikuwa zikitokea kwa sababu hawakuwa wakifuatana na walezi. Tumejaribu kupamba eneo hili na hata kutafuta nafasi ya vyoo vya muda. Hata hivyo, kinachowafanya watu waondoke na wasirudi tena ni harufu ya majitaka. Wengine hufika majini lakini hawaingii kwa sababu wanaona maji ni machafu,” alisema Bw Mangale. Alieleza kuwa baadhi ya watalii hutembelea eneo hilo na kubaki kufurahia mandhari ya bahari pekee. “Tuna chama ambacho wawekezaji wanaweza kushirikiana nacho ili kuhakikisha jamii inanufaika. Nina matumaini kuwa hili likifanyika, ufukwe wetu hatimaye utaanza kuvutia,” alisema Bw Mangale. Serikali ya Kaunti ya Mombasa ilisema kuwa inatambua kuhusu hali ya fukwe zilizo ndani ya kisiwa. Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi na Mipango ya Miji katika kaunti Mohamed Hussein, kaunti ina mipango ya kukarabati fukwe hizo ili kutumia kikamilifu uwezo wao. “Kwa sasa tunashughulikia tatizo la majitaka kwa kuhakikisha kuwa majengo mapya yote Mombasa yanawekewa ‘biodigester’. Hii itahakikisha kuwa maji yanayotolewa kutoka kwenye majengo hayo hayadhuru tena mazingira,” alisema. Aliongeza kuwa, idara hiyo inajenga kituo cha kusafisha majitaka kitakachohakikisha kuwa maji yote yanayoelekezwa baharini ni safi. “Fukwe zina uwezo wa kuwaunganisha watu na hata kubadilisha maisha; ndiyo maana tunafanya kazi bila kuchoka kuondoa vikwazo vinavyozuia ufuo wetu kustawi. Tunataka wananchi wetu wafurahie fukwe, ndiyo maana maafisa wa afya ya umma tayari wako mashinani wakichukua hatua,” alisema Bw Hussein. Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli na Wahudumu wa Migahawa nchini, Dkt Sam Ikwaye, fukwe za Mombasa ni miongoni mwa vivutio vikuu katika eneo hili. Hata hivyo, usimamizi duni, kanuni zinazokinzana na mgawanyiko usio wazi wa majukumu kati ya serikali ya kitaifa na kaunti vimezuia matumizi kamili ya rasilimali hizi. “Ni vigumu kubaini ni nani ana jukumu la kuwekeza katika miundomsingi, usalama wa fukwe na maendeleo yake,” alisema Dkt Ikwaye. Mwenyekiti huyo wa Baraza la Utalii la Mombasa, alisema kuwa jitihada zimefanywa kuandaa kanuni zitakazoongeza thamani ya fukwe zinazotumika tayari pamoja na zile ambazo bado zimetelekezwa. “Kupitia chama cha wahudumu wa hoteli, tumeweza kushirikiana na serikali ya kaunti ya Kwale pamoja na serikali ya kaunti ya Mombasa. Kufikia sasa, tayari tumewasilisha rasimu za sheria za usimamizi wa fukwe katika kaunti hizi,” alisema Dkt Ikwaye.