MBUNGE wa zamani wa Taveta, Bw Basil Criticos na Mama Ngina Kenyatta sasa wanapambana kupata hatimiliki ya ardhi ya ekari 2,536 katika Kaunti ya Taita Taveta. Ekari hizo ni zile zilizosalia baada ya kuuza sehemu ya ardhi hiyo kwa Rais William Ruto mnamo 2017, wakati huo Ruto akiwa naibu rais. Wakati huo, Bw Criticos alikuwa akiandamwa na kesi nyingi kortini. Baada ya kumuuzia Rais ardhi hiyo, alitumia hatimiliki ya ardhi kupata mkopo wa Sh200 milioni kutoka benki. Hata hivyo, kinaya ni kwamba miaka minane baadaye, Bw Criticos pamoja na mmiliki mwenzake Mama Ngina Kenyatta bado wako mahakamani. Wanasaka haki ya kuamrisha Wizara ya Ardhi iwape hatimiliki ya ardhi yenye ekari 2,624 zilizosalia baada ya kumuuzia Rais Ruto. Stakabadhi za mahakama zinaonyesha kuwa Wizara ya Usalama wa Ndani inalenga kugawanya ardhi hiyo ambayo imesajiliwa chini ya Bw Criticos na Bw Kenyatta. Ardhi hiyo inagawanywa ili kuwapa makao maskwota wa Jipe/Kachero, hatua inayoonyesha hatima tofauti kwa vipande viwili vya ardhi ambavyo vilikuwa chini ya umiliki mmoja. Siku nne kabla ya Bw Criticos kupata amri ya pili ya korti iliyoagiza Wizara ya Ardhi kumpa na Bi Kenyatta cheti kipya cha umiliki wa ardhi, Rais Ruto alibatili uteuzi wake kwenye Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Kibiashara Kenya (KenTrade). Aliondolewa miezi mitano kabla ya muhula wake kutamatika mnamo Aprili 30 2026. Juhudi za kufahamu iwapo kufutwa kwa Bw Criticos kwenye bodi hiyo kulihusishwa na vita vyake na Kenya Kwanza kuhusu ardhi hiyo, ziligonga mwamba. Hii ni kwa sababu idara au kitengo cha mawasiliano cha rais hakikujibu kufikia wakati wa kuchapisha habari hizi. Mnamo 2022, Bw Criticos na Bi Kenyatta bado walikuwa wakipambana na Wizara ya Ardhi kortini kuhusu madai ya wizara kuwa ekari 2624 zilikuwa zimepewa serikali miaka kadhaa nyuma kuwapa maskwota makao. Rekodi za korti zinaonyesha hatimiliki ya ardhi hiyo ilitolewa kwa Jonathan Kiraga ambaye alidai yeye ni wakili wa Bw Criticos. Hata hivyo, miaka miwili baadaye imebainika kuwa Bw Criticos hakuwa na wakili kama huyo na huenda hatimiliki ilikuwa imeibwa. Pia kwenye sajili ya Chama cha Mawakili Nchini (LSK) hakuna wakili ambaye anaitwa Jonathan Kiraga.