SIKUKUU za Krismasi na Mwaka Mpya ni siku mbili zinazobeba uzito mkubwa katika jamii ya Wakenya. Ni nyakati za shukrani, mapumziko na kuimarisha mahusiano ya kifamilia. Hata hivyo, sherehe hizi mara nyingi huambatana na changamoto za kiusalama, kimaadili, kiuchumi na hasa usafiri barabarani. Ni wajibu wa kila Mkenya kusherehekea kwa busara ili furaha ya leo isigeuke kuwa majuto ya kesho. Kwanza kabisa, suala la usalama ni la msingi. Wakati huu hushuhudia ongezeko la uhalifu, ajali na hata migogoro ya kifamilia. Ni vyema wananchi wawe waangalifu wanapohama makwao au kusafiri kwenda kusherehekea na jamaa zao. Milango na mali vihifadhiwe vyema, watoto wasiachwe bila uangalizi, na kuepuka maeneo hatari hasa nyakati za usiku. Sherehe hazipaswi kudhuru maisha. Pili, maadili hasa miongoni mwa watoto na vijana hayapaswi kusahaulika. Likizo ndefu huwaachia watoto uhuru mkubwa ambao bila uangalizi unaweza kuwaangamiza kimaadili na hata kuwaharibia maisha. Wazazi na walezi wanapaswa kutumia muda huu kuwakaribia watoto wao, kuwafundisha maadili mema, kuwahusisha katika shughuli za kifamilia na kijamii, na kuwazuia kujitosa katika mienendo mibaya kama matumizi ya dawa za kulevya, pombe na tabia zisizofaa. Krismasi si msimu wa kulegeza maadili, bali wa kuyaimarisha. Tatu, usafiri barabarani ni jambo linalohitaji umakinifu wa hali ya juu. Kila mwaka, tunapoteza mamia ya maisha kutokana na ajali zinazoweza kuzuilika. Madereva wanapaswa kuzingatia sheria za trafiki, kuepuka mwendo wa kasi, kutoendesha wakiwa wamelewa na kuhakikisha magari yako katika hali nzuri. Hatimaye, suala la matumizi ya fedha ni la busara kubwa. Sherehe zisigeuke mashindano ya anasa na ubadhirifu. Ni vyema kukumbuka kuwa Januari huja na mahitaji mengi, ikiwemo karo za shule, kodi, na gharama za kila siku. Mkenya mwenye hekima husherehekea kulingana na uwezo wake, akitenga akiba ya kutosha kwa majukumu ya baada ya sikukuu. Furaha ya siku chache haipaswi kuwafanya watoto wakose masomo au familia iingie kwenye madeni yasiyo ya lazima. Hitimisho, Krismasi na Mwaka Mpya ni nyakati za baraka na matumaini. Tusherehekee kwa amani, kwa usalama, kwa maadili mema na kwa nidhamu ya kifedha. Tukifanya hivyo, tutaanza mwaka mpya tukiwa na afya, heshima na matumaini mapya badala ya vilio na majuto.