LONDON, UINGEREZA SAUDI Arabia imetekeleza adhabu ya kifo kwa watu 347 katika mwaka huu wa 2025, wengi wao wakiwa raia wa kigeni, kwa makosa mbalimbali yanayohusiana na dawa za kulevya, kulingana na shirika la Reprieve linalofuatilia adhabu za vifo. Katika ripoti yake ya hivi punde, shirika hilo, lenye makao yake Uingereza, linaeleza kuwa miongoni mwa walionyongwa ni wanawake na mwanahabari mmoja. Hali hiyo, kulingana na shirika hilo, inayoonyesha ongezeko la maafa yanayotokana na hatua ya Saudi Arabia kuendelea kutekeleza adhabu za kifo katika vita vyake dhidi ya ulanguzi wa mihadarati. Hata hivyo, kulingana na Reprieve, thuluthi mbili ya walionyongwa ni wale waliopatikana na makosa yanayohusiana na dawa zisizo na madhara makubwa, hatua ambayo Umoja wa Mataifa (UN) inataja kama “isiyolingana na taratibu na viwango vya kimataifa. “Aidha, jumla ya watu 96 walionyongwa walihusishwa na dawa za kulevya aina ya hashish,” shirika hilo linaeleza kwenye ripoti hiyo iliyotolewa Jumapili. Familia za wanaonyongwa kwa makosa kama hayo nchi Saudi Arabia huwa hazifahamishwi mapema kabla ya adhabu hiyo kutekelezwa, haziruhusiwi kuchukua miili ya wapendwa wao na huwa hawafahamishwi kuhusu mahala pa mazishi. Serikali ya nchi hiyo pia huwa haifichui mbinu zinazotumika kutekeleza adhabu hiyo ya kifo, japo inaaminika mbinu inayotumika zaidi ni ukataji vichwa na kupigwa risasi. Ongezeko visa vya wahalifu kunyongwa nchini Saudi Arabia inafuatia hatua ya nchi hiyo kuondoa marufuku dhidi ya utekelezaji wa adhabu hiyo mwishoni mwa 2022. Afisi ya Umoja wa Mataifa ya kutetea haki za kibinadamu ilitaja hatua hiyo kama ya “kusikitisha zaidi.” “Saudi Arabia sasa inakiuka sheria kiholela. Imedharau kanuni inayozihitaji nchi zote kuheshimu haki za kibinadamu,” akasema Jeed Basyouni, mkuu wa kitengo cha adhabu ya kifo katika shirika la Reprieve, anayesimamia Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini. Bi Basyouni aliongeza kuwa visa vya washukiwa kuteswa na kulazimishwa kukiri makosa vimekithiri zaidi nchini Saudi Arabia, kando na raia wasio na hatia na watu wasiojiweza kudhulumiwa. “Inaonekana kuwa hawatakiwa kujua ni nani wanayemnyonga, mradi wamepitisha ujumbe kwa jamii kwamba hawavumilii makosa mbalimbali, kama vile kushiriki maandamano kinyume cha sheria au ulanguzi wa dawa za kulevya,” akaeleza afisa huyo wa shirika la Reprieve. Mwanamfalme Mohammed bin Salman, ambaye alitwaa mamlaka ya uongozi katika nchi hiyo mnamo 2027, ameanzisha mageuzi ya kijamii, yakiwemo kuhusu wanawake kuendesha magari, kupunguza mamlaka ya polisi wa kidini na kufungua nchi hiyo kwa uwekezaji. Lakini licha ya uwepo wa mabadiliko hayo, makundi ya kutetea haki za kibinadamu, ikiwemo Human Rights Watch (HRW), yanaendelea kueleza kuwa rekodi ya Saudi Arabia katika kuheshimu haki za kibinadamu iko chini zaidi huku idadi ya wanaonyongwa ikikaribia ile ya nchi za China na Iran.