Polisi watibua maandamano Ikulu ya Nairobi

POLISI wa kupambana na ghasia jana walitawanya familia za wahanga wa maandamano ya Gen-Z ambao walikuwa wakiandamana kuelekea Ikulu ya Nairobi. Waandamanaji hao walitaka kuzungumza na Rais William Ruto kuhusu kuchelewa kupata haki kwa wahanga wa maandamano yaliyofanyika 2024-2025. Maandamano hayo yalikuwa yamepangwa na wazazi na jamaa wa vijana waliouawa katika maandamano ya hapo awali. Hasa wazazi hao walilalamikia kukosa kupata haki na fidia kutokana na mauti na majeraha ya watoto wao. Video iliyosambaa mitandaoni iliwaonyesha waandamanaji hao wakipeperusha bendera na kubeba maua huku wakielekea barabara ya Ikulu. Walipokaribia ikulu walirushiwa gesi ya kutoza machozi na wakatawanyika huku wingu la moshi likitanda.