MKENYA aliyeokoka kunyongwa Saudi Arabia kimuujiza na kurejea nyumbani baada ya miaka 14 akiwa jela amesema atamuoa mpenzi wake raia wa Afrika Kusini ambaye hakumtoroka katika kipindi hicho. Stephen Betrand Munyakho aliyefahamika kama Abdulkareem, 51, alifungwa mnamo 2011 baada ya kupigana na mfanyakazi mwenzake nchini Saudia, tukio lililosababisha kifo. Wanawake watatu waliendelea ‘kusimama’ naye katika masaibu hayo, na sasa anasema ndio watu anaowaenzi mno. Mmoja ni mama yake, nyanya yake na mpenzi wake raia wa Afrika Kusini. Bw Munyakho alikuwa amefanya kazi nchini humo kwa muda wa miaka 15 kabla ya kufungwa. “Mamangu, nyanyangu na mpenzi wangu hawakunitoroka. Walinipa matumaini kuwa mambo yangekuwa mazuri na ikatokea hivyo,” akasema Bw Munyakho. Kati ya watatu hao, masikitiko makuu ni kuwa nyanyake tayari ameaga dunia. “Alikuwa ameahidi kusakata densi kwa mguu wa tatu (mkongojo) iwapo ningerejea. Hata hivyo, nilirudi kama ameaga dunia,” akaongeza. Mamake, Dorothy Kweyu, ambaye ni mhariri na mwandishi ana umri unaozidi miaka 70, na alikuwa katika uwanja wa ndege wa JKIA kumpokea aliporejea mnamo Julai 29. Tangu Juni 2014 aliposukumiwa adhabu ya kifo, alikuwa akisubiri siku ambayo jina lake lingeitwa na chakari ili aende anyongwe. Kuhusu mpenzi wake, Bw Munyakho alisema ni tabibu ambaye anaishi jijini Johannesburg. “Ni mwanamke wa kipekee na amekuwa nami kwa zaidi ya miaka 14 bila kutetereka,” akasema. Alifichua kuwa mpenzi wake huyo hangefika Kenya Julai kumkaribisha kwa sababu alikuwa na majukumu mengi kazini. “Ninatamani sana kukutana naye tena na kumwona uso kwa macho. Iwapo uhusiano huu haungekuwa na hatima ya ndoa, basi sidhani kama bado ungekuwa unaendelea kwa kipindi hiki chote,” akasema. Simulizi yake inalandana na ya aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela ambaye alikaa gerezani miaka 27 huku muda huu wote mkewe Winnie Mandela akimsubiri. “Yetu ni nusu ya ile ya Mandela,” akasema. Kabla ya kufungwa, Bw Munyakho alikuwa baba wa watoto watatu ambao wana umri wa miaka 32,30 na 25. Watoto hawa aliwapata na mpenzi wake wa zamani kabla ya kukutana na huyu wa Afrika Kusini ambaye anapanga kumwoa. Familia yake, serikali, Chama cha Wahariri na Wakenya Saudia Arabia walikuwa na kibarua kigumu kuhakikisha kuwa wanachangisha Sh150 milioni ambazo zilifahamika kama ‘pesa za damu’ ili kumwokoa. Iwapo pesa hizo hazingepatikana, familia ya mwanaume, raia wa Yemen, aliyeaga baada ya kuzozana na Bw Munyakho ilitaka anyongwe kulingana na sheria za Kiislamu. Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu nchini (SUPKEM), Hassan ole Naado alitangaza kuwa Muungano wa Mataifa ya Kiislamu Duniani (MWL) ulitoa Sh129 milioni ili kumwokoa Bw Munyakho.