BAADA ya wenyeji Morocco kutandika Comoros 2-0 katika gozi la ufunguzi wa Kombe la Afrika (AFCON) 2025 mnamo Jumatatu usiku, leo itakuwa zamu ya Senegal, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Nigeria na Tunisia pia kudhihirisha ubabe wao. Mabao ya Morocco waliokuwa wakicheza katika uwanja wa Prince Moulay Abdellah jijini Rabat yalifumwa wavuni kupitia kwa Brahim Diaz na Ayoub El Kaabi. Senegal leo watavaana na Botswana katika uga wa Grand Stade de Tanger, kila mmoja akianza kampeni zake za AFCON katika Kundi D akiwa na matarajio tofauti. DR Congo nao watamenyana na Benin katika pambano jingine la Kundi D uwanjani Al Barid. Nigeria watafungua michuano ya Kundi C dhidi ya Tanzania uwanjani Fez, saa chache kabla ya Tunisia kushuka dimbani kukwaruzana na Uganda ugani Olympique Annexe Complexe Sportif Prince Abdellah. Tofauti na Senegal wanaopigiwa upatu wa kutwaa taji la AFCON 2015, Botswana watashuka dimbani wakisaka ushindi wa kwanza kwenye fainali za kipute hicho. Wakiwa miongoni mwa timu zenye uzoefu zaidi barani Afrika, hii ni mara ya 18 kwa Senegal kunogesha AFCON na ya sita mfululizo kwa mabingwa hao wa 2021. Katika safari ya kufuzu, miamba hao walitandaza mechi sita bila kupoteza huku wakiruhusu wapinzani kuwafunga bao moja pekee. Safu yao ya uvamizi itaongozwa na Sadio Mane kwa ushirikiano na Habib Diarra, Ismaila Sarr na Cheikh Sabaly. Senegal watajibwaga ugani wakiwa na motisha tele baada ya kupepeta Uingereza 3-1 kirafiki mwezi Juni ugani Nottingham City Ground kabla ya kupigwa na Brazil 2-0 mnamo Novemba kisha wakacharaza Kenya 8-0. Kihistoria, Senegal wanajivunia rekodi nzuri katika mechi za ufunguzi wa AFCON, wakisalia bila kushindwa katika mechi 15 kati ya 17 za mwanzo wa mashindano hayo huku wakitawala mechi zao tano zilizopita. Leo itakuwa mara ya kwanza kwa Senegal kukutana na Botswana katika fainali za AFCON, baada ya kuwalaza mara mbili wakati wa kampeni ya kufuzu kwa AFCON 2015 kwa kuwashinda 2-0 ugenini Septemba 2014 kisha 3-0 nyumbani mnamo Novemba 2014. Nigeria wanalenga kupiga hatua moja zaidi baada ya kutinga fainali ya AFCON 2023. Ikizingatiwa kwamba kumekuwepo na washindi saba tofauti katika makala manane yaliyopita ya AFCON, fainali za mwaka huu zinatarajiwa kuibua msisimko mkubwa. Morocco ndiyo timu inayopewa nafasi kubwa zaidi ya kunyanyua ufalme ikizingatiwa kwamba iko kwenye ardhi ya nyumbani na ndicho kikosi bora zaidi barani Afrika tangu kiweke historia ya kutinga nusu-fainali ya Kombe la Dunia mnamo 2022. Chini ya kocha Walid Regragui aliyeshuhudia Morocco wakibanduliwa katika hatua ya 16-bora kwenye AFCON 2023, kibarua kikubwa zaidi mara hii ni kuhimili presha. Matarajio ya mashabiki wao jijini Rabat ni kwamba kikosi chao kitatwaa taji la AFCON mnamo Januari 18, 2026; kwa mara ya kwanza tangu 1976. Miamba wengine wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda AFCON ni Afrika Kusini ambao wamekuwa wakitamba chini ya kocha Hugo Broos, aliyeongoza Cameroon kutwaa taji la 2017. Algeria nao wanajivunia mfungaji bora katika mechi za kufuzu kwa AFCON 2025, Mohamed Amoura, ambaye alipachika wavuni mabao 10. Anatarajiwa kuongoza kikosi hicho cha Afrika Kaskazini kutinga hatua ya muondoano kwa mara ya kwanza katika makala matatu yaliyopita. Sawa na Botswana na Msumbiji, Tanzania pia wanasaka ushindi wao wa kwanza kwenye AFCON – na wanalenga kutinga hatua ya muondoano kwa mara ya kwanza – kadri wanavyojiandaa kuwa wenyeji wa fainali za 2027 pamoja kwa pamoja na Kenya na Uganda. Huku mabingwa 12 wa zamani wakiwa uwanjani mara hii, nafasi ya kikosi kipya kuibuka mfalme wa AFCON 2025 ni finyu sana japo chochote huenda kikatokea. RATIBA YA AFCON (LEO): DR Congo vs Benin (3:30pm) Senegal vs Botswana (6:00pm) Nigeria vs Tanzania (8:30pm) Tunisia vs Uganda (11:00pm)