Korti yazima kuuzwa kwa shamba la wakili wa ICC aliyepatwa amekufa 2022

MAHAKAMA Kuu imezuia kuuzwa kwa shamba moja la hadhi jijini Eldoret linalomilikiwa na marehemu wakili Paul Gicheru. Hatua hiyo imefufua mzozo kuhusu umiliki wa mali ya wakili huyo aliyehusishwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) jijini Hague, Uholanzi. Mzozo huo ni kati ya mjane Ruth Nyambura na Ian Njoroge ambaye anadai yeye ni mwanawe marehemu, akidai umiliki wa shamba hilo. Bi Nyambura alimrejelea Bw Njoroge, 26, kama mtu asiyemfahamu ambaye hata hakuwa kwenye ratiba ya mazishi ya marehemu. Bw Njoroge naye anasema kuwa marehemu alimpa ardhi hiyo akiwa yungali hai. Ametumia cheti chake cha kuzaliwa ambacho kina jina la Bw Gicheru kuthibitisha kuwa marehemu ni babake. Bi Nyambura anataka kuuza ardhi hiyo kufadhili masomo ya wanawe wawili ambao wako katika chuo kimoja nchini Uingereza. “Mshtakiwa anasema kuwa anahitaji pesa hizo kugharimia elimu ya wanawe. Naye aliyewasilisha kesi hiyo anasema atapoteza mali yake,” ikasema mahakama. Kwenye uamuzi ambao unaonekana kumfaa Bw Njoroge, Jaji Helene Namisi aliondoa amri ya awali ya korti ambayo ilikuwa imeruhusu mauzo ya shamba hilo. Bw Gicheru ambaye alikuwa wakili aliaga dunia mnamo Septemba 6, 2022. Alipata umaarufu kutokana na ICC kumshutumu kwa kuvuruga ushahidi kwenye kesi iliyowasilishwa kortini humo baada ya ghasia za uchaguzi wa 2007/8. Alikanusha madai hayo na kujiwasilisha kwa korti mnamo 2020 japo aliaga dunia kabla ya kesi kuanza kusikizwa.