SASA barabara zinazoelekea nyumbani kwa Kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka katika eneo la Mwingi Kaskazini zitawekwa lami baada ya majibizano makali kati yake na Rais William Ruto wiki hii. Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi wa Barabara Kuu (KeNHA) imewaalika wanakandarasi watume maombi ya kuweka lami katika barabara ya Kandwia-Kyuso na ile ya Kyuso-Tseikuru. Kwenye notisi, KeNHA ilisema wanakandarasi wanatarajiwa kutembelea barabara hizo katika kituo cha kibiashara cha Kandwia mnamo Januari 15, 2026 kabla ya kufunguliwa kwa tenda mnamo Februari 5 kwenye makao makauu ya KeNHA Nairobi. “Mamlaka inawaalika wanakandarasi kutuma ombi la kutengeneza barabara hizo,” ikasema sehemu ya notisi iliyotiwa saini na naibu mkurugenzi wa KeNHA anayehusika na utoaji zabuni. Hatua hiyo inakuja wakati cheche kali na joto la kisiasa linaendelea kupanda kati ya Rais Ruto na Bw Musyoka kuhusu hali ya barabara hizo. Rais Ruto na wandani wake wamekuwa wakimrejelea Bw Musyoka kama kiongozi asiyechangamkia maendeleo kutokana na hali duni za barabara hizo licha ya kuwa uongozini kwa miaka 40. Bw Musyoka analenga kuwania urais mnamo 2027 kupitia Wiper Patriotic Front. Rais amekuwa akishangaa jinsi Bw Musyoka ataendeleza taifa kama alilemewa kutengeneza barabara za kuelekea kwake licha ya kuwa uongozini kwa kipindi kirefu. “Wakenya wanastahili kuwakataa viongozi ambao hawana rekodi ya maendeleo kwa sababu kila kitu unachofanya lazima kianzie nyumbani. Kama hawawezi kuendeleza vijiji na maeneo wanakotoka basi hawawezi kufanya hivyo kwa Wakenya,” akasema Mbunge wa Mwala, Vincent Musyoka kwenye mkutano wa kisiasa Nairobi hivi majuzi. Bw Musyoka hata hivyo ametetea rekodi yake ya maendeleo akisema amefanya mengi kwa zaidi ya miaka 40 aliyokuwa kwenye utumishi wa umma. Akihojiwa majuzi na NTV, alidai ndiye aliasisi kuwekwa lami kwenye barabara ya Kibwezi-Kitui ambayo inafikia nyumbani kwake wakati ambapo alikuwa makamu wa rais katika utawala wa marehemu Rais Mwai Kibaki.