ZIMWI la ajali jana liliendelea kuwatafuna Wakenya baada ya watu tisa kufariki kwenye ajali mbili tofauti huku ulimwengu ukiadhimisha Sikukuu ya Krismasi leo. Zaidi ya watu wanane walipoteza maisha yao huku wengine saba wakijeruhiwa vibaya kufuatia ajali mbaya ya barabarani kwenye kituo cha kibiashara cha Mukhonje katika eneobunge la Lugari usiku wa kuamkia Jumatano. Desemba 24, 2025. Ajali hiyo ilifanyika kwenye barabara kuu ya Eldoret-Webuye na ilihusisha matatu na lori lililokuwa likisafirisha mbolea. Mkasa huo ulisababisha wingu la huzuni kwa wenyeji na wenye magari huku kila moja akifanya juhudi za kuwasaidia walioumia. Walioshuhudia ajali hiyo walisema matatu ilikuwa ikielekea Webuye kutoka Eldoret na ikagongana na lori ambalo lilikuwa limeegeshwa kando ya barabara. Katika Kaunti ya Nakuru watu wawili akiwemo dereva wa lori waliaga dunia kwenye ajali mbaya ya barabarani eneo la Sachangwan katika barabara ya Nakuru-Eldoret. Zaidi ya watu 10 ambao walipata majeraha mabaya kwenye ajali hiyo nao watakula Krismasi wakiwa hospitalini. Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Trafiki Kaunti ya Nakuru Allan Ogolla, ajali hiyo ilihusisha magari matano ikiwemo gari aina ya Nissan Matatu lililokuwa likiwasafirisha abiria kutoka Eldoret. “Dereva wa lori alikuwa akielekea Nakuru na akashindwa kudhibiti gari. Aliaga dunia na abiria aliaga kutokana na majeraha akiendelea kupokea matibabu katika Hospitali ya Kaunti ndogo ya Molo,” akasema Bw Ogolla. “Wale ambao walijeruhiwa walikimbizwa hadi Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Molo na ile ya Rufaa na Mafunzo ya Nakuru wanakoendelea kupokea matibabu,” akaongeza. Magari yaliyohusika kwenye ajali hiyo yalikokotwa hadi Kituo cha polisi cha Molo. Walioshuhudia ajali hiyo walisema ni kama lori lilikuwa na matatizo ya kiufundi na dereva akashindwa kulidhiti kabla halijagonga gari jingine. “Dereva wa lori alikuwa akiendesha kwa kasi ya juu kabla ya ajali kufanyika. Hii ndiyo maana ilikuwa vigumu sana kwake kulidhibiti kabla ya kugongana na gari jingine,” akasema James Kinuthia ambaye alishuhudia ajali hiyo. Tukio hilo la mapema asubuhi lilivuruga trafiki kwenye barabara hiyo yenye shughuli nyingi. Polisi na wahudumu kutoka kwa Shirika la Msalaba Mwekundu walikuwa wakijaribu kuendeleza juhudi za uokoaji. Kufuatia ajali hiyo Kamishina wa Ukanda wa Bonde la Ufa Dkt Abdi Hassan alitoa wito kwa wanaotumia barabara kuhakikisha wanadumisha nidhamu na kufuata sheria za trafiki. “Polisi zaidi na maafisa wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama Barabarani (NTSA) wametumwa katika barabara mbalimbali kuhakikisha kuna nidhamu na hatupotezi maisha zaidi. Nawaomba sote tumakinike barabarani na maisha ya kila anayetumia barabara lazima yalindwe,” akasema Dkt Hassan.