Nyoro: Mimi si fuko na sikuunga mkono utimuaji wa Gachagua

MBUNGE wa Kiharu, Ndindi Nyoro amezungumza kwa mara ya kwanza na kufafanua kwa nini alihepa kikao cha kumngátua aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, akisema mchakato huo haukuongozwa na hekima. Bw Nyoro ambaye amekuwa vuguvugu kuhusu uungwaji mkono wake kwa serikali na pia hajaonyesha hadharani anaegemea mrengo wa Bw Gachagua, pia amefichua kuwa uhusiano wake na Rais William Ruto umesambaratika kabisa. Kwenye mahojiano na Inooro, mbunge huyo alisema utathmini wa kina haukufanyika kuhusu athari na udhaifu wa kumfurusha Bw Gachagua. “Nilitoa ushauri kuhusu utathmini wa jinsi suala hilo lingeathiri watu na kwamba kumwondoa kutegemea ufafanuzi kuhusu matokeo ya tukio hilo. Kwa masikitiko hakuna aliyenijali,” akasema Bw Nyoro. Hoja ya kumbandua Bw Gachagua iliwasilishwa bungeni na Mbunge wa Kibwezi Mashariki Mwengi Mutuse na ikafaulu mnamo Oktoba mwaka jana. “Nilishauri kwamba tofauti za kimawazo zingetatuliwa kuliko tofauti za kibinafsi. Utathmini mbaya ulifanyika na sasa tuko hapa,” akaongeza. Nyota ya kisiasa ya Bw Nyoro ilikuwa imeanza kungáa baada ya Rais Ruto kuapishwa uongozini mnamo Septemba 13, 2022. Wakati ambapo Bw Gachagua alikuwa akibanduliwa, kulikuwa na gumzo kwamba Bw Nyoro alikuwa kati ya wale ambao wangerithi nafasi yake. Kutokana na kimya chake cha kipindi kirefu, wengi walikuwa wakiamini kwamba Bw Nyoro alikuwa kati ya waliokuwa wamesuka mpango wa kumtimua Bw Gachagua. Pia kumekuwa na minongóno kwenye upinzani kwamba yeye ni fuko wa Rais Ruto. Hata hivyo, Bw Nyoro sasa anasema hakuna ndoa yoyote ya kisiasa kati yake na Rais Ruto. Hii ni licha ya Rais kumiminia sifa kedekede kama mwanasiasa anamkuza wakati wa ziara yake ya siku sita ukanda wa Mlima Kenya mnamo Aprili 1, 2025. Bw Gachagua naye hivi majuzi alimtaka Bw Nyoro kutangaza msimamo wake wa kisiasa. “Kunyamaza kwako hakusaidii kwa sababu tunataka kujua idadi yetu na masuala ya jamii si ya wanasiasa wanaokimya,” akasema Bw Gachagua.