Wetang’ula ahimiza amani, upendo Krismasi

Spika wa Bunge la Taifa,Moses Wetang’ula amewataka Wakenya kutafakari na kukumbatia amani na upendo wakati wa sherehe za Krismasi. Spika Wetang’ula amesema Krismasi hii inamkumbusha kuwa nuru ya kweli haitangazi ujio wake, bali huangaza kimya kimya. “Ni wakati wa tafakari nzuri, wa kung’aa, kwa unyenyekevu na kukumbatia upendo na amani,” alisema Wetang’ula. Amesema taifa linapaswa kukumbatia kiini cha Krismasi, akibainisha kuwa ni wakati unaojawa na upendo na shukrani. “Katika kuchagua unyenyekevu, upendo hupata maana; katika kukumbatia ukimya, roho hugundua amani. Nakaribisha msimu huu takatifu kwa shukrani na matumaini,” alisema. Spika aliwahimiza Wakenya waendelee kulindana na kuwa waangalifu wanapokuwa katika maeneo ya umma. “Tuungane kama familia na jamii moja kubwa tunapoadhimisha Krismasi na kufurahia matumaini yanayoambatana na Mwaka Mpya,” alihimiza Spika Wetang’ula.