JANGA la kibinadamu linaendelea kuongezeka Angata Barikoi, Trans Mara, Kaunti ya Narok baada vita vya kijamii vilivyosababisha mauti ya watu nne. Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Eliud Lagat alitangaza kafyu eneo hilo kutokana na kuchacha kwa mapigano kati ya jamii hizo. Wakimbizi waliotoroka makabiliano wanaendelea kuhangaika huku wakikosa mahitaji ya kimsingi, vyakula, maji na hata dawa. Familia hizo sasa zinaishi kwenye shule na vituo vya polisi. Kwa mujibu wa Mshirikishi wa Shirika la Msalaba Mwekundu Ukanda wa Kusini mwa Bonde la Ufa, Felix Maiyo, hali ni mbaya na familia hizo zinastahili kusaidiwa. “Hatuna chakula cha kutosha na pia bidhaa nyinginezo. Tunahitaji chakula cha kuwapa watoto na watu wanaoishi na aina mbalimbali ya ulemavu,” akasema Bw Maiyo. “Wakenya wanaposherehekea Krismasi, tunaomba waonee familia hizi zinazohangaika na kuwapa misaada,” akaongeza. Wengi bado wanahofia kurejea nyumbani kwao wakiogopa kuvamiwa. Bw Maiyo ameomba vyombo vya usalama vihakikishe kuwa hakuna mauaji zaidi eneo hilo. Baadhi ya waliothirika walisema kuwa wameishi eneo hilo tangu wazaliwe na ghasia hizo zimesambaratisha maisha yao. Edna Chelangat sasa anaishi Shule ya Msingi ya Kondamet baada ya kuvamiwa nyumbani kwake eneo la Orgilai. “Nahisi kwamba sina chochote na hata sielewi kwa nini niko hapa. Nimepoteza kila kitu,” akasema mama huyo, 56 wa watoto saba.