DCI yatengua kitendawili cha probox katika ajali ya Jirongo

Maafisa wa upelelezi wanaochunguza kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Lugari, Cyrus Jirongo, wamefanikiwa kufuatilia gari aina ya Toyota Probox ya rangi nyeupe lililonaswa na kamera za CCTV katika kituo cha mafuta kilicho karibu na eneo la ajali, na tayari wamerekodi taarifa kutoka kwa waliokuwa ndani ya gari hilo . Aliyekuwa Mbunge wa Lugari alifariki dunia baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani huko Karai, kwenye barabara kuu ya Nairobi–Nakuru, katika saa za alfajiri za Desemba 13, 2025. Katika ripoti iliyotolewa kupitia akaunti yake rasmi ya X siku ya Alhamisi, Desemba 25, 2025, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ilisema kuwa timu ya maafisa wa upelelezi ilisafiri hadi Keringet, eneo la Kuresoi Kusini, Kaunti ya Nakuru, kuwahoji watu wanaohusishwa na gari hilo. “Katika uchunguzi unaoendelea kuhusu mazingira ya kifo cha Mheshimiwa Cyrus Jirongo, aliyefariki baada ya kupata majeraha katika ajali mbaya ya barabarani, timu ya maafisa wa upelelezi ilisafiri hadi Keringet, Kuresoi Kusini, Kaunti ya Nakuru, kuwatafuta na kuwahoji watu wanaohusishwa na gari jeupe lenye nambari za usajili KDJ 564E, Toyota Probox ,” DCI ilisema. Gari hilo lilinaswa na kamera za CCTV katika Kituo cha Mafuta cha Eagol, likiingia muda mfupi baada ya marehemu kuingia na kutoka usiku wa ajali hiyo. Kwa mujibu wa DCI, taarifa zilirekodiwa kutoka kwa wahusika waliothibitisha kuwa gari hilo limesajiliwa kwa jina la Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kaunti ya Nakuru, William Mutai, ambaye pia ni Mwakilishi wa Wadi ya Keringet, na kwamba gari hilo linasimamiwa na mke wake. DCI ilieleza kuwa Desemba 11 2025, mke wa Mutai alikodisha gari hilo kwa Denis Kipyegon Koech, aliyekuwa na nia ya kusafirisha watu wafamilia kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kumpokea mwana wao aliyekuwa akirejea kutoka Chuo Kikuu cha New Mexico nchini Amerika. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Koech na familia yake waliondoka Keringet kuelekea Nairobi Desemba 12 2025, na kufika JKIA saa tano usiku. Ndege aliyosafiria mwana wao ilitua takriban saa kumi usiku, na baada ya kukamilisha taratibu za ukaguzi, familia ilianza safari ya kurejea Keringet muda mfupi baada ya saa sita usiku. DCI iliripoti kuwa walipofika Karai wakiwa safarini , eneo la ajali, walisimama katika Kituo cha Mafuta cha Eagol kujaza maji ya kifaa cha kusafisha kioo. “Ni kwa muda mfupi waliosimama ambapo, walimwona marehemu akitoka katika kituo hicho na kuelekea upande wa Nairobi. Muda mfupi baadaye, walipokuwa wakijaza maji hayo, walisikia mlio mkubwa na kuona basi likivuta gari la marehemu,” DCI ilisema. Kwa mujibu wa maelezo waliyotoa kwa maafisa wa upelelezi, baada ya kumaliza kujaza maji, familia hiyo ilitoka katika kituo cha mafuta na kusimama kwa muda mfupi karibu na eneo la ajali kwa ombi la mlinzi wa kituo hicho, aliyewaomba wasaidie katika juhudi za uokoaji. DCI ilisema hawakushuka kutoka ndani ya gari lao, bali walitumia taa za gari kuangazia eneo la ajali kwani kulikuwa na giza na magari mengine yalikuwa bado hayajafika. “Waliondoka eneo la ajali baada ya magari mengine kuanza kufika na msongamano wa magari kuanza kujitokeza, wakaendelea na safari yao na kufika nyumbani takriban saa kumi na mbili asubuhi, ambako baadaye walipata habari kwamba mwathiriwa wa ajali hiyo alikuwa Mheshimiwa Cyrus Jirongo,” taarifa hiyo ilisema. DCI ilisisitiza kuwa wachunguzi wanaendelea kuchunguza ukweli wa madai yaliyotolewa na waliokuwa ndani ya gari hilo. “DCI inaendelea kuchunguza ukweli wa madai hayo na inahakikishia familia, marafiki na wananchi wa Kenya kwamba uchunguzi wa kina na usio na upendeleo kuhusu tukio hili unaendelea,” idara hiyo ilihitimisha.