KATIKA mtandao wa kijamii wa Truth Social, Rais wa Amerika, Donald Trump alisema kuwa nchi yake imeanzisha mashambulizi makali dhidi ya ISIS Kaskazini-Magharibi mwa Nigeria, ambao wamekuwa wakiwalenga na kuwaua Wakristo wasio na hatia. “Marekani imeanzisha mashambulizi makali dhidi ya ISIS Kaskazini-Magharibi mwa Nigeria, ambao wamekuwa wakiwalenga na kuwaua kikatili Wakristo wasio na hatia,” Trump aliandika katika mtandao wa kijamii wa Truth Social. Tukio hili la hivi punde linajiri wakati hali ya ukosefu wa usalama ikiongezeka katika nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika, ambayo imekuwa ikikabiliwa na ghasia kwa miaka kadhaa. Kundi la kigaidi la Kiislamu la Boko Haram lina mizizi yake nchini Nigeria pia. Mapema mwezi Novemba Trump alionya kwamba Washington inaweza kuhusika katika mashambulizi hayo, akitoa wito kwa serikali ya Nigeria kuzuia vifo zaidi na kutishia kwamba isipofanya hivyo itakabiliwa na kupunguzwa kwa misaada. Hata hivyo, ghasia zimeendelea, huku takriban watu watano wakiuawa na 35 kujeruhiwa katika shambulio la bomu la kujitoa mhanga kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo, msemaji wa polisi katika eneo hilo alisema siku ya Alhamisi, Desemba 25, 2025. Kufuatia shambulio hilo la Marekani katika Siku ya Krismasi, Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth amesema "anashukuru kwa msaada na ushirikiano wa serikali ya Nigeria." Kwa mujibu wa Kamandi ya Marekani ya Afrika, walengwa walikuwa katika jimbo la Sokoto la Nigeria.