RAIS William Ruto na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta wamejipata ndani ya mzozo ambao unatishia kusambaratisha ODM kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Mirengo inayozozona ndani ya ODM sasa inalaumiana kuhusu madai ya kuuza chama hicho kwa Rais Ruto na Bw Kenyatta kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao. Viongozi wa ODM wanaounga mkono Serikali Jumuishi wamedai kuwa kuna njama ya kurejesha chama upinzani kwa kuinadi kwa Bw Kenyatta ambaye ni kiongozi wa Jubilee. Hata hivyo, wale wanaopinga ushirikiano wa ODM na serikali wamezungumzia mpango wa kuuza chama kwa Rais Ruto. ODM kwa sasa inaonekana imebaki yatima baada ya kifo cha Kinara wake Raila Odinga ambaye alihakikisha udhabiti wake kwa miaka 20 aliyoiongoza tangu ibuniwe. Kambi ambayo inapinga chama kushirikiana na Rais ni Katibu Mkuu Edwin Sifuna, Naibu Kiongozi wa chama Godfrey Osotsi na Gavana wa Siaya James Orengo. Upande unaorindima ngoma ya Rais Ruto una Kiongozi wa ODM wa sasa Dkt Oburu Oginga, Mwenyekiti Gladys Wanga na Magavana Abdulswamad Nassir na Simba Arati ambao wanashikilia wadhifa wa naibu kiongozi wa ODM pamoja na Mkurugenzi wa uchaguzi chamani Junet Mohamed. Akiongea katika eneobunge lake la Suna Mashariki, Bw Mohamed ambaye ni kiongozi wa wachache bungeni alidai kuwa rais mstaafu ana mkono fiche na anaunga mkono baadhi ya viongozi wanaolenga kusambaratisha ODM. Bw Mohamed alisimulia jinsi ambavyo kiongozi mmoja alimuita kwenye kikao cha saa nane usiku hoteli moja jijini Kisumu kumshawishi ODM iuzwe. Mwanasiasa huyo alimfahamisha kuhusu ahadi kutoka kwa Bw Kenyatta iwapo ODM ingeondoa uungwaji mkono kwa Rais Ruto. Alisema kiongozi huyo alimjia na mpango na mbinu za kutumika kujiondoa kwenye Serikali Jumuishi kwa kutaja kutotekelezwa kwa hoja 10 zilizoko kwenye muungano wa ODM na UDA. “Aliniambia Rais Mstaafu anataka kusaidia ODM na yuko tayari kuwekeza zaidi ya Sh1 bilioni chama ili tushinde uchaguzi kwa kuungana na upinzani,” akadai Bw Mohamed. “Kama Uhuru alikuwa na vyombo vya mamlaka na hakufanya Raila awe rais, sasa ndio ataweza sasa?” akauliza. Bw Mohamed alisema kiongozi aliyempa habari hizo ni kati ya wale ambao wamekuwa wakipiga kelele na kupinga ushirikiano na Rais Ruto. “Umekuwa ukisema tunataka kukiuza chama kwa Ruto na sasa unataka tukiuze kwa Uhuru. Sasa sisi ni mabroka wawili waliokaa hapa. Tuite mabroka na wezi lakini hatutaondoka kwenye Serikali Jumuishi na ni wewe utaondoka ODM, "Tumechoka kupashwa na watu waliojiunga na ODM kutoka ANC na kama una shida, nenda ukabuni chama chako ila hatutawapeleka watu wetu njia hiyo unayoitaka,” akasema Bw Mohamed. Juhudi za kupata kauli ya Bw Kenyatta kuhusu madai yaliyotolewa dhidi yake hazikuwa zimefua dafu wakati wa kuchapisha habari hizi. Msemaji wake Kanze Dena hakuwa amejibu simu au jumbe alizotumiwa kufikia wakati wa kuchapisha habari. Bw Nassir akizungumza katika eneobunge la Likoni siku mbili zilizopita alidai kuwa mrengo unaompinga Rais Ruto unataka kufilisi ODM ndani kwa ndani. “Nataka kuwaambia kuwa hawatafaulu kwa sababu watu wametuambia hakuna kukaa upinzani tena. Raila hakufaa ili tuendelee kuwa upinzani,” akasema. Mbunge huyo wa zamani wa Mvita alidai kuwa kuna watu ambao wapo ODM mchana na usiku wanafanya juu chini kuhakikisha chama kinasambaratika. “Wengine wanaojifanya wanapenda chama hata walimsaliti Raila na wanazungumzia ODM vibaya usiku. Hatutoki Serikali Jumuishi na tunawajua wale ambao wanapanga kusambaratisha chama,” akasema gavana huyo. Kinaya ni kwamba madai ya Bw Mohamed yanakuja siku chache baada ya Mabw Sifuna na Orengo kudai kulikuwa na mpango wa kunadi ODM kwa Rais Ruto. “Tunasema kuwa ODM haiuzwi na kama umedanganywa na wale ambao umewalipa pesa za mwanzo kuwa umeuziwa chama, fahamu wamekulaghai,” akasema Bw Sifuna kwenye mkutano wa kisiasa Magharibi mwa Kenya. “Hatujamtuma yeyote kujadiliana kwa niaba ya ODM. Hatujamtuma broka na mtu kama huyo ni mlaghai ambaye anataka kukulaghai,” akaongeza. Bw Osotsi naye amesisitiza kuwa ODM haitamuunga Rais Ruto iwapo muafaka wao na UDA hautatekelezwa. Seneta huyo alisema Rais ana hadi Machi 2026 kuonyesha kile ambacho ametekeleza la sivyo asahau uungwaji mkono wao. “Bila hiyo hakuina muafaka kwa sababu uungwaji mkono wa ODM unapewa kwa kufanya yanayotakikana na raia,” akasema Bw Osotsi.