SERIKALI ya Kenya Kwanza inapanga kukarabati Barabara ya Ikulu ya Nairobi kwa gharama ya Sh1.6 bilioni. Taarifa zilizomo katika notisi ya zabuni iliyotolewa Desemba 19 zimeorodhesha kazi zilizokusudiwa kuwa sehemu ya miradi 92 ya ukarabati wa barabara nchini kote. Serikali imekadiria kuwa miradi hiyo itagharimu takriban Sh15.6 bilioni kwa jumla. Hati hiyo, iliyotiwa saini na Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Barabara za Mijini (KURA), inaelezea zabuni hiyo kama hatua ya kuimarisha ubora wa Barabara ya Ikulu." Barabara hiyo ni muhimu sana kwani inaunganisha CBD na maeneo muhimu kama vile Ikulu na afisi za serikali zilizo karibu. Polisi mara nyingi wamelazimika kuimarisha usalama na kuzuia watu kufika eneo hilo hasa wakati wa maandamano kama vile maandamano ya Gen Z ya 2024 dhidi ya Mswada wa Fedha. Mnamo Oktoba mwaka huu, afisa wa Kitengo cha Utumishi Mkuu (GSU) anayelinda Ikulu aliuawa wakati raia alipomvamia kwa mshale karibu na lango, na kusababisha wasiwasi kuhusu usalama katika eneo hilo. Kando na Barabara ya Ikulu, zabuni nyingine iliyoorodheshwa kugharimu zaidi ya Sh1 bilioni ni ujenzi wa Barabara ya Chelimo katika Mji wa Kericho kwa gharama inayokadiriwa ya Sh1.1 bilioni. Miradi yote itafadhiliwa na Serikali ya Kenya chini ya KURA. "Ili kuimarisha usawa, walengwa watawasilisha zabuni zisizozidi mbili (2), lakini wanaweza tu kupewa kiwango cha juu cha zabuni moja (1), chini ya notisi hii ya zabuni. Wale watakaotuma zabuni zaidi ya mbili (2) wataondolewa," notisi hiyo inasema kwa sehemu. Miradi mingine muhimu ya barabara iliyoorodheshwa ni pamoja na ukarabati wa barabara za Mji wa Gede-Kakuyuni katika Kaunti ya Kilifi kwa gharama ya Sh967.5 milioni, ujenzi wa barabara kuu za Eldoret City kwa Sh950 milioni, na uunganishaji wa barabara ya Oginga Odinga kutoka Subukia hadi mzunguko wa Westmall katika Kaunti ya Nakuru kwa gharama ya Sh850 milioni. Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya alitaja miradi hiyo katika Kaunti ya Kilifi kuwa hatua ya mabadiliko katika eneo hilo, akisema imekuwa ikitengwa kwa miongo mingi.