IDARA ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) imewataka Wakenya wakome kueneza uvumi kuhusu chanzo cha kifo cha mbunge wa zamani wa Lugari, Bw Cyrus Jirongo. Mkurugenzi wa DCI, Bw Mohamed Amin, alisema uchunguzi uliofanywa kufikia sasa umeonyesha chanzo cha kifo hicho kilikuwa ni ajali ya barabarani, ingawa uchunguzi zaidi unaendelezwa. “Hili ni tukio linaloendelea kuchunguzwa. Hadi sasa, uchunguzi unaonyesha kuwa ilikuwa ajali ya barabarani,” alisema akiwa Diani, Kaunti ya Kwale mnamo Alhamisi. Wakati uo huo, Bw Amin aliwahakikishia Wakenya usalama wao wakati wa msimu wa sikukuu, akisema hali ya usalama nchini kwa ujumla ni shwari licha ya visa vichache vya uhalifu na migogoro ya kijamii katika baadhi ya maeneo. Bw Amin alisema kuwa polisi wameongeza doria na operesheni za kijasusi kote nchini ili kulinda wananchi na wageni. “Tumeona ongezeko la baadhi ya visa vya kikatili, vikiwemo mauaji na biashara ya dawa za kulevya, lakini hali inadhibitiwa. Usalama wa wananchi ni suala ambalo tumelipa kipaumbele,” alisema Bw Amin. Alikiri kuwepo kwa changamoto za kiusalama katika maeneo ya Trans Mara na Tana River, akisema vimedhibitiwa kwa sasa. Tayari Trans Mara, polisi wamewakamata washukiwa watano wanaodaiwa kuhusika na kuchochea ghasia, hali iliyosababisha kupungua kwa uhasama. Katika Kaunti ya Tana River, washukiwa watano walikamatwa kuhusiana na ghasia ambazo zimekuwa zikiibuka mara kwa mara. Bw Amin aliwataka wakazi wa Tana River wanaomiliki silaha haramu kuzisalimisha kwa hiari na haraka iwezekanavyo. “Nawasihi wote wenye silaha haramu katika eneo hilo wazisalimishe kwa hiari ili kurejesha amani ya kudumu ama hatua zitachukuliwa dhidi yao,” alisisitiza. Mkuu huyo wa DCI pia alitaja kukamatwa kwa maafisa wa polisi wa trafiki na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kama njia moja ya kupambana na ufisadi nchini. EACC ilikamata maafisa wawili wa trafiki Jumanne, katika barabara ya Likoni-Lungalunga wakidaiwa kuitisha hongo kutoka kwa wenye magari. “Hatutavumilia ufisadi wa aina yoyote. Hatua kali na za kisheria zitachukuliwa dhidi ya afisa yeyote atakayepatikana akijihusisha na vitendo vya ufisadi,” aliongeza. Aliwahimiza wananchi wazidi kuwa makini na kuripoti mienendo yoyote ya kutiliwa shaka, akisema maafisa wa polisi wako kazini saa 24 kwa siku kote nchini. Vyombo vya usalama vimesema doria zilizoboreshwa na ushirikiano wa karibu na jamii utaendelea kuimarishwa kipindi chote cha sikukuu.