POLISI Migori wanaendelea kuwazuilia washukiwa watatu kuhusiana na kifo cha mwanajeshi wa kike wa KDF ambaye alipatikana ameuawa mkesha wa sikukuu ya Krismasi nyumbani kwake kijiji cha Nyahera, Suna Mashariki. Polisi kutoka Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) waliwakamata watatu hao kusaidia kwenye uchunguzi wa kifo cha afisa huyo, Luteni Cynthia Awuor Mboya, 28. Afisa huyo huhudumu katika Kituo cha wanajeshi cha Gilgil. Wale ambao wanazuiliwa kutokana na mauti ya Bi Awuor ni mumewe, mkwe wake na shemeji yake. Wachunguzi walipata nguo ambayo inadaiwa ilivaliwa na marehemu wakati wa kuuawa kwake. Panga, ambayo inadaiwa ilitumika kutekeleza mauaji hayo pia ilipatikana. Luteni Mboya alikuwa amesafiri nyumbani kwa mapumziko kipindi hiki cha likizo ili kuungana na mumewe kwa sherehe za Krismasi. Alikuwa anatarajiwa arejee Gilgil lakini sasa amepoteza maisha kupitia njia tatanishi. Maafisa wa usalama kutoka Kituo cha Polisi cha Migori waliitia wito wa mumewe na kupata mwanajeshi huyo akiwa amelala kwenye chumba chake. Uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa alikuwa amekatwa puani na kulikuwa na dalili kuwa alinyongwa. Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, mume wake alisema hakuwa nyumbani wakati mauaji hayo yalitokea. Aliwaambia polisi kuwa alifunga duka lake saa saba usiku na aliporejea nyumbani alipata mlango umefunguliwa. Alipoingia chumba cha kulala ndipo aliupata mwili wa mkewe kitandani kisha akapiga ripoti kwa naibu chifu ambaye aliwaarifu polisi. Kamanda wa Polisi wa Suna Mashariki Samuel Boit alisema kuwa Naibu Chifu wa Osingo Calvis Odeka alifahamishwa kabla yake kuwaarifu maafisa wa usalama. Bw Boit aliongeza kuwa mume huyo pia alisema simu mbili za mkono za marehemu zilikuwa zimepotea. Anaendelea kuzuiliwa ili kusaidia uchunguzi unapoendelea.