Mnara wa ukumbusho kwa heshima ya waliopoteza maisha wakipinga utawala wa kikoloni utajengwa eneo la Chetambe, Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, amesema . Akizungumza wakati wa Tamasha la Utamaduni wa Tachoni lililofanyika katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro, Spika Wetang’ula alisema serikali imejitolea kujenga mnara huo katika eneo la ekari 20, ambao utakuwa kitovu cha historia na utalii wa kitamaduni. Wakati huo huo, Spika Wetang’ula ametoa wito kwa madereva na watumiaji wa barabara kuzingatia kikamilifu sheria za usalama barabarani ili kukomesha ajali zinazozidi kugharimu maisha ya wananchi, hasa wakati wa msimu wa sikukuu. Spika alisema hayo jana alipokuwa Kaunti ya Bungoma, alipoongoza ujumbe wa wabunge kutoa pole kwa familia iliyopoteza watoto watatu katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea mkesha wa Krismasi. Akiandamana na Kiranja wa Wengi katika Seneti, Seneta Wafula Wakoli, Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Bungoma, Catherine Wambilyanga, na Mbunge wa Webuye Mashariki, Martin Pepela, Spika alitembelea familia ya Mzee Samson Barasa katika eneo la Sipala, Kaunti Ndogo ya Webuye Mashariki. Watoto hao walikuwa miongoni mwa watu 12 waliopoteza maisha katika ajali iliyotokea eneo la Mukhonje kwenye barabara kuu ya Webuye–Malaba. Marehemu ni Walter Simiyu aliyekuwa anatarajiwa kujiunga na Kidato cha Nne, Humphrey Muriithi aliyekuwa mwanafunzi wa Darasa la Sita, pamoja na Prince Baraka. Walikuwa wakirejea nyumbani kusherehekea Krismasi na familia yao ajali hiyo ilipotokea. Akizungumza kwa masikitiko makubwa, Mzee Barasa alisema msiba huo umeacha pengo kubwa katika familia yake. “Awali nilidhani ni ndoto mbaya, lakini nilipotambua ukweli, moyo wangu ulivunjika kabisa. Tulikuwa tumejiandaa kusherehekea Krismasi pamoja kama familia,” alisema. Akielezea msiba huo kuwa mzito kwa familia, Spika Wetang’ula alisema ajali za barabarani zinaendelea kuangamiza ndoto na mustakabali wa vijana wengi nchini. “Huu ni ushahidi wa gharama inayotokana na uzembe na uendeshaji magari usiozingatia sheria, hasa wakati wa sikukuu,” alisema. Aliwahimiza madereva kuacha mwendo wa kasi, kutoendesha magari wakiwa wamelewa na kuheshimu sheria zote za barabarani ili kuzuia vifo vinavyoweza kuepukika. Kwa upande wake, Seneta Wakoli alitoa wito kwa Serikali ya Kaunti ya Bungoma kuongeza ufadhili wa shughuli za kitamaduni, akisisitiza kuwa masuala ya utamaduni ni jukumu la serikali za kaunti. Viongozi hao waliwahimiza wakazi kudumisha amani na umoja wanapokaribisha Mwaka Mpya.