Afisa mmoja wa polisi ameripotiwa kufariki dunia, raia kadhaa kujeruhiwa na pikipiki mbili kuchomwa moto huko Kibiko, Kaunti Ndogo ya Kajiado Magharibi, kufuatia mvutano unaoendelea kuhusu ardhi ya kijamii . Afisa huyo aliyeuawa alikuwa miongoni mwa maafisa kadhaa waliojeruhiwa baada ya kundi la vijana waliozua ghasia kuwavizia maafisa wa polisi wa kawaida na wa Kikosi cha Kukabi na Fujo(GSU), Alhamisi, Sikukuu ya Krismasi, wakitoa ulinzi kwa wapima ardhi waliokuwa wakiweka alama. Aidha, raia kadhaa walipata majeraha wakati wa makabiliano hayo huku watu saba wakikamatwa na kwa sasa wanazuiliwa na polisi wakisubiri kufikishwa mahakamani Jumatatu. Inadaiwa kuwa vijana waliokuwa wamejihami kwa mishale, mikuki na silaha walikuwa wakishirikiana na baadhi ya viongozi wa eneo hilo wanaopinga ugawaji wa ardhi hiyo. Pikipiki mbili zilichomwa moto usiku uliopita kabla ya waendesha pikipiki hao kushambuliwa kwa mapanga. Wamo miongoni mwa waliolazwa kupokea matibabu katika hospitali mbalimbali. Ulinzi umeimarishwa ili kuhakikisha zoezi la kuweka alama za kugawa ardhi linaendelea bila kukatizwa. Chanzo cha mvutano ni ugawaji wa kipande cha ardhi cha ekari 2,800 cha thamani ya Sh100 bilioni huku migogoro ya uongozi ikiweka makundi mawili hasimu katika mzozo wa muda mrefu uliokwamisha zoezi hilo kwa miaka. Kundi moja linaloungwa mkono na serikali ya Kaunti ya Kajiado linaongozwa na mwenyekiti wa muda mrefu Moses Parantai, huku kundi jingine lililojitenga likiongozwa na Moses Monik. Kila upande una idadi kubwa ya wanachama. Kundi linalotekeleza zoezi la kugawa ardhi linaloongozwa na Moses Monik, alipokuwa akihutubia wanahabari Kibiko Jumamosi, lilidai kuwa ndilo uongozi halali unaotambuliwa na serikali na uko tayari kutoa hati miliki kwa wanachama wote. Monik alidai kuwa wanaopinga mchakato unaoendelea waliuza hisa zao kwa watu wa nje miaka mingi iliyopita, lakini akasisitiza kujitolea kwake kuhakikisha hakuna mwanachama anayefukuzwa au kunyimwa sehemu yake. “Mapigano ya hivi karibuni yalifadhiliwa na wanasiasa wa eneo hili na watu wachache waliouza hisa zao kwa wageni ili kukwamisha mchakato. Wanaogopa kuwa utoaji wa hati miliki za mtu binafsi utaweka wazi njama zao,” alisema Monik. “Hivi karibuni tumetoa angalau hati miliki 4,000 kwa wanachama wetu. Hatutaruhusu kuvurugwa katika kuhakikisha hakuna mwanachama atakayefukuzwa au kupoteza haki yake ya umiliki wa ardhi.” Aliwakemea baadhi ya viongozi wa eneo hilo aliowatuhumu kwa kufadhili vijana kusababisha vurugu. “Tunahimiza maafi wa usalama kuvunja makundi ya wanaowatesa wanachama wasio na hatia. Katika mwezi mmoja uliopita, watu wamekatwa viungo na mali kuchomwa. Haya lazima yakomeshwe,” aliongeza Bw Monik. Katibu Mkuu wa Kibiko Community Land Trust, Emmanuel Litei, alisema ulinzi wa polisi katika zoezi hilo ni kutambuliwa kwa timu yao kupitia taasisi mbalimbali za serikali. “Zoezi hili limechelewa kwa muda mrefu. Sisi (kundi letu) tunazo nyaraka zote zinazohitajika za serikali kutekeleza zoezi hili. Nawapa changamoto wapinzani wetu watoe nyaraka zao ziwekwe wazi kwa umma,” alisema Bw Litei. Zoezi hilo linatarajiwa kukamilika wiki ijayo. Mnamo Ijumaa, Seneta wa Kajiado Samuel Seki, akifuatana na Waziri wa Kaunti (CEC) anayesimamia masuala ya ardhi Hamilton Parseina, walitembelea eneo hilo kabla ya kulaani vurugu hizo. “Baadhi ya maafisa wakuu wa serikali wanajitahidi kwa nguvu kunyakua sehemu ya ardhi ya jamii. Waonywe, hatutaruhusu wachukue hata inchi moja ya ardhi ya mababu wetu,” alisema Seneta Seki. Kamanda wa Kaunti ya Kajiado, Alex Shikondi, amewaonya watu wanaochochea vurugu kwa maslahi ya kibinafsi, akisema idara za usalama zilikubali kutoa ulinzi baada ya kuchunguza nyaraka zilizowasilishwa na kundi linaloweka mipaka. “Wajibu wetu (polisi) ni kutoa ulinzi. Hatutaruhusu uvunjaji wa sheria. Baadhi ya wanasiasa na watu binafsi wanachunguzwa na polisi kwa uchochezi. Watakaopatikana na hatia watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Shikondi.