Zaidi ya watu 100,000 wajitokeza kuwania kura ya UDA Mlimani na Bonde la Ufa

ZAIDI ya wanachama 100,000 wa UDA wametuma maombi ya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa mashinani ambao umepangwa kuanza Januari 2026 Mlima Kenya na Bonde la Ufa. Idadi hiyo inatarajiwa kupanda zaidi baada ya chama kuongeza muda wa kujisajili hadi Disemba 31, 2025. Takwimu kutoka Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi zilionyesha kuwa wengi Mlima Kenya na Bonde la Ufa wanasaka uongozi UDA. Vyama hivyo vilimuunga mkono Rais Ruto kwa dhati katika uchaguzi wa 2022. Mwenyekiti wa Bodi ya Uchaguzi Anthony Mwaura alisema kuwa wanachama 14,700 kule Uasin Gishua, 9037 kutoka Nyandarua, 2113 kule Tharaka-Nithi na wanachama 5,014 Embu wametuma maombi kuongoza UDA kwenye uchaguzi kwenye kituo cha kupiga kura maeneo hayo mnamo Januari 10. Kaunti nyingine ambazo zimeshuhudia idadi ya juu ni Nyeri (4,131), Kakamega (4,656), Bomet (4,212), Nakuru (5,036), Nandi (5,102), Murang’a (3,390), Trans Nzoia (4,067), Vihiga (4,193), Meru (5,060), Baringo (6,084), Kiambu (8,027), Kirinyaga (3,081), Kericho (3,024), Laikipia (4,028), Elgeyo Marakwet (4,184) na Samburu (5,000). Kwenye uchaguzi wa kituoni, chama kitawachagua maafisa 20. Kwa mujibu wa mwongozo wa uchaguzi, idadi hii itashirikisha wawakilishi watatu wa makundi ya kidini, wawakilishi wanne wa wafanyabiashara, wasomi watatu, vijana wanne, mtu mmoja kutoka makundi spesheli, wakulima watatu na wanachama wawili wanaowakilisha wanawake na wanaume. UDA ilianza chaguzi zake za mashinani mnamo Aprili 2024 lakini ikaahirisha chaguzi hizo kutokana na maandamano ya Gen Z. Awali Busia na Homa Bay zilimaliza chaguzi zao. Mnamo Aprili 2025 UDA iliandaa chaguzi za mashinani kwenye kaunti 22 na sasa shughuli hiyo imeandaliwa kwenye kaunti 27 kwa jumla. Awamu ya mwisho ya uchaguzi kwenye kituo cha kupiga kura zitaandaliwa kwenye kaunti 20 zilizosalia. Idadi ya wanaojitokeza na wanaowania chaguzi za UDA Mlima Kenya itakuwa na umuhimu kupima iwapo chama hicho bado ni maarufu eneo hilo. Baadhi ya waliokuwa wandani wa Rais Ruto eneo hilo 2022 washahamia kambi ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na wanaunga mkono chama chake cha DCP. “Kuna ushindani mkali kwenye nyadhifa mbalimbali Mlima Kenya na Bonde la Ufa,” akasema Bw Mwaura. Kutokana na uhasama kati ya Rais Ruto na Bw Gachagua, chama hicho bado kilikuwa kinahofia kuandaa chaguzi hizo ndogo. Hata hivyo, ushindi kwenye uchaguzi mdogo wa Mbeere Kaskazini unaonekana umewaashajisha katika eneo ambalo wengi walikuwa wakifikiria lishajiondoa serikalini. Kaunti 10 za Mlima Kenya na saba za Bonde la Ufa zilimpa Rais Ruto jumla ya kura milioni 4.5 ambazo ni asilimia 63 za kura zote alizopata. Kaunti za Laikipia, Tharaka Nithi, Murang’a, Kiambu, Nyeri, Kirinyaga, Nyandarua, Embu, Meru na Nakuru zilichangia Rais karibu kura milioni tatu huku saba za Bonde la Ufa zikimpa kura milioni 1.6.