Kampuni 70 za maji kufungwa sababu ya deni la Sh25B

KAMPUNI za maji 70 huenda zikafungwa huku zikiandamwa na madeni na kukadiria hasara ya zaidi ya Sh25 bilioni, ripoti mpya imefichua. Ripoti hiyo iliweka wazi jinsi mashirika hayo ya utoaji huduma yamesakamwa na deni la Sh20.3 bilioni, hali ambayo imesababisha sehemu kubwa ya kampuni hizo 87 kufilisika. Ripoti hiyo iliyotolewa na Afisi ya Bajeti ya Bunge (PBO) ilifichua kuwa asilimia 86 ya kampuni hizo 87 za maji zinakabiliwa na misukosuko ya kifedha ziking’ang’ana na madeni. Kampuni hizo zilipoteza Sh5.1 bilioni katika mwaka mmoja pekee kupitia maji yaliyosambaziwa wateja lakini hayakulipishwa katika mwaka wa bajeti iliyokamilika Juni 30, 2024; hivyo kuhatarisha ustawishaji wa kifedha wa kampuni nyingi zinazotoa huduma za kusambaza maji katika kaunti. Ripoti hiyo inasema hali iliyopo inaashiria utepetevu wa serikali, kukosa nidhamu kifedha, na utendakazi duni. PBO inaashiria kuwa asilimia 86 ya kampuni za maji ziliendesha shughuli zake zikiwa zimelemewa kifedha, kutokana na kukosa mtaji kwa sababu zimeshindwa kukusanya Sh15.3 bilioni zinazodai. Hali hii ilizidishwa na hasara ya kila mara kutokana na maji yasiyolipiwa, mipangilio ya kodi iliyopitwa na wakati na gharama za juu. Hata hivyo, ni kampuni 12 pekee za maji zilizorekodi nafasi bora ya mtaji pasipo kuashiria matatizo kifedha. Kampuni ya maji ya Nairobi, kulingana na ripoti hiyo, inajumuisha sehemu kubwa ya kiasi cha Sh5.3 bilioni, ikifuatiwa na Kampuni za Maji Mombasa, Sh2.2 bilioni na Malindi. Kampuni za Maji za Tavevo (Sh965.35 milioni), Nakuru (Sh683.6 milioni), Kakamega (Sh671.9 milioni), Kwale (Sh618.6 milioni) na Kilifi Mariakani (Sh506 milioni) zinafuata kwa mzigo wa madeni. Kampuni nyingine 14 zina deni la zaidi ya Sh200 milioni nyingine 20 zikipambana na deni la zaidi ya Sh100 milioni. Kampuni nyingine 10 za maji zinakadiria hasira kati ya Sh51 milioni na Sh98 milioni, 16 zinadaiwa kati ya Sh21.7 milioni na Sh45 milioni huku sita zikidaiwa zaidi ya Sh10 milioni. Ni kampuni za Maji ya Cherang’any Marakwet na Marsabit pekee zinazodaiwa chini ya Sh1 milioni. “Kushindwa kukidhi gharama ya oparesheni kunahatarisha pakubwa kuendeleza huduma na kuhujumu haki ya kupata maji kikatiba,” inasema ripoti.