RAIS William Ruto atashinda muhula wa pili mamlakani iwapo uchaguzi wa urais ungefanyika hivi leo, hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na kampuni ya Infotrak. Kulingana na utafiti huo kwa jina ‘End-Year Poll Politics’, Rais Ruto anaongoza kwa umaarufu kwa asilimia 23 akifuatwa na aliyekuwa Waziri wa Usalama Fred Matiang’I ambaye ametangaza kuwania kiti hicho (asilimia 13) naye Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ataibuka wa tatu kwa asilimia 12. Hata hivyo, kutawazwa mshindi kwa kura ya urais nchini ni sharti mwaniaji apate asilimia 50+1 ya kura halali zilizopigwa kwa sababu hiyo, inamaanisha kwamba kungehitajia awamu ya pili ya kura iwapo matokeo yakuwa kama yalivyotabiriwa na utafiti huo. Rais William Ruto ameonekana kupanda kwenye umaarufu haswa baada ya kuridhia kufanya kazi na aliyekuwa Waziri Mkuu marehemu Raila Odinga, hali iliyosaidia kudhibiti serikali yake iliyokuwa inakumbwa na msukosuko uliochangiwa na maandamano ya Gen Z 2024. Umaarufu wake unaonekana kuchupa zaidi kufuatia ushindi mnene kwenye uchaguzi mdogo ambapo wawaniaji wa Serikali Jumuishi kwenye ngazi za useneta na ubunge wote walishinda viti walivyowania; jambo lililopokeza kipigo kikali kwa mrengo wa upinzani unaojumuisha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka na Fred Matiang’i.