Msitumie akiba yote kwa sherehe za sikukuu, ‘Njaanuari’ ndio ilee… yaja

KRISMASI na Mwaka Mpya huja na shamrashamra nyingi, mapochopocho, wageni, safari na zawadi. Kwa wanandoa wengi, ni kipindi cha kuonyesha upendo na ukarimu. Hata hivyo, kuna haja wanandoa wawe waangalifu hasa ikija katika suala la kutumia pesa. Kumbuka kuwa kusherehekea zaidi na kutumia fedha nyingi kufurahia Desema kuna maadhara, hasa mwezi wa Januari ukifika. Katika harakati za kufurahisha familia na marafiki, baadhi ya wanandoa hutumia akiba yote waliyoweka mwaka mzima. Wanakula, wanakunywa na kusafiri kana kwamba mwaka unaishia Disemba. Matokeo yake ni mwezi wa Januari uliojaa msongo wa mawazo, madeni na migogoro ya kifamilia. Mtaalamu wa masuala ya fedha Stephen Okoth anawashauri wanandoa kutumia pesa vizuri wakati huu wa sherehe. “Tatizo si kusherehekea, bali ni kukosa mipango ya baada ya sherehe,” anasema mshauri wa masuala ya fedha, Bw Okoth. Anaeleza kuwa Januari huja na majukumu mbalimbali kama vile karo, kodi ya nyumba, ununuzi wa chakula na kulipa madeni ya Disemba. Bila akiba, shinikizo huongezeka na mara nyingi huathiri mahusiano ya wanandoa. Kwa mujibu wa Bw Okoth, baadhi ya wanandoa husherehekea kwa kulinganisha maisha yao na ya wengine. Wanakopa ili wasionekane wameachwa nyuma au wanatumia zaidi ya uwezo wao ili kuwafurahisha wageni. “Sherehe si mashindano. Furaha ya kweli ni amani ya nyumbani, si sifa za nje,” anasema. Mbali na hayo, anawanashauri wanandoa wakubaliane mapema kuhusu bajeti ya sherehe na waweke mipaka ya matumizi. Sehemu ya akiba inapaswa kubaki kwa matumizi ya Januari. Badala ya safari za gharama au sherehe za kifahari, wanandoa wanaweza kuchagua kusherehekea nyumbani, kupika pamoja na kushirikisha watoto katika shughuli nyepesi lakini zenye maana. “Watoto hawahitaji sherehe kubwa; wanahitaji upendo pamoja na muda wa pamoja na wazazi wao,” anasema Bw Okoth. Anasisitiza kuwa sherehe za busara huwafundisha watoto nidhamu ya kifedha na umuhimu wa kupanga maisha. Japo siku hizo mbili – Krismasi na Mwaka Mpya – huja mara moja kila mwaka, bado kuna maisha baada ya sherehe hizo. Kubakisha akiba kidogo husaidia familia kuanza mwaka mpya kwa matumaini, si kwa lawama na majuto. “Hekima ya sherehe ni kufurahia leo bila kuharibu kesho,” anasisitiza Bw Okoth. wonyando@ke.nationmedia.com