KAMPENI za uchaguzi mkuu wa 2027 tayari zinaendeshwa siyo kwenye majukwaa ya hadhara bali katika mitandao ya kijamii. Mwaka huu mawimbi ya jumbe za kisiasa yalivuma kwenye mtandao wa X (zamani twitter) yakilenga wanasiasa mbalimbali nchini na makabila fulani. Uchanganuzi ulioendeshwa na “Trust Lab”- mradi unaoendeshwa na mashirika ya DW Akademie (DWA), Code for Africa na Siasa Place , chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya- unafichua uwepo wa kampeni ya kusambaza taarifa za kupotosha zinazolenga kuvuruga imani, kuchochea migawanyiko na ajenda mbalimbali. Taarifa hizo siyo propaganda za kawaida, bali zile zinazolenga kuwaharibia watu fulani heshima na kuvunja ngome mbalimbali za kisiasa. Kampeni hizo za kueneza taarifa za kupotosha mitandaoni zinaendeshwa kwa kutumia akaunti mbalimbali zenye muingiliano fulani, ishara kwamba zimepangwa kwa hali ya juu. Operesheni hizi pia zimejitokeza kupitia hashtegi za kusuta jamii ya Agikuyu na viongozi wenye ushawishi kama vile aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. Kampeni kali kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii mwaka huu, zilizovutia zaidi hasa katika jukwaa la X zililenga kuvunja nguvu za kisiasa za eneo la Mlima Kenya. Dhana iliyolengwa kuendelezwa ni kwamba jamii ya Agikuyu, Aembu na Ameru (GEMA) zinapoteza nguvu kisiasa na viongozi wao ndio wa kulaumiwa kwa hilo. Hii ilijitokeza kwenye kampeni kupitia hashtegi #SmallVotesBigDamage iliyoendeshwa kati ya Juni 5 na Juni 9, 2025. Kampeni hiyo ilitajwa mara 6,172 na kusomwa zaidi ya mara 163,000 na kuvumisha dhana kwamba nguvu za kisiasa zinazotokana na wingi wa watu kutoka jamii kubwa hazipo. Wahusika katika uendeshaji wa kampeni hii walighushi stakabadhi kuthibitisha madai yao. Moja kati ya stakabadhi hizo ilidaiwa kutoka kwa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) ikionya kuhusu hatari ya kusambaratika kwa umoja wa kisiasa wa jamii za GEMA. Stakabadhi nyingine feki ilidaiwa kutoka kwa Shirika la International Foundation for Electoral Systems (IFES), ikidai kuwa ushawishi wa wapigakura sasa umeelezwa kwa “kujitokeza kwa wingi” kwa watu kutoka kaunti zenye idadi ndogo ya watu. Ujumbe huo ulishadidiwa na hashtegi kama vile #43against1 iliyoshuhudiwa kati ya Januari 20 na Januari 25 mwaka huu iliyoweka nchi hizo dhidi ya jamii ya Agikuyu. Kampeni hii ilisomwa na zaidi ya watu 113,000 na ililenga Bw Gachagua na wandani wake kama vile Seneta wa Nyandarua Methu John Muhia, Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba, na Seneta wa Kiambu Karungo Paul Thang’wa. Kampeni hiyo ililenga kutenga eneo la Mlima Kenya, hasa jamii ya Agikuyu, na Wakenya wengine kwa maslahi ya waendesha kampeni hiyo. Vile vile, kampeni kupitia hashtegi #MukimoMafia iliyotajwa mara 5,867 iliendeleza dhana kwamba wakereketwa wa imani ya "Itungati" wanalenga kutenganisha Mlima Kenya na maeneo mengine ya nchi. Waendeshaji kampeni hiyo pia walisambaza habari kwenye kurasa za mbele za magazeti zikihusishwa Gachagua na kundi fulani la kigaidi. Mbinu hiyo ililenga kusawiri viongozi wa eneo la Mlima Kenya kama wanaohusika na makosa ya uhaini. Maandamano ya kupinga serikali yalipotokea mnamo Juni 2025, waendesha habari za kupotosha mitandaoni walikuwa wepesi kudai kuwa maandamano hayo yalichochewa kisiasa. Kampeni kupitia hashtegi #TheLordOfViolence iliyoendeshwa kati ya Juni 25 hadi Julai 8 ililenga kuendeleza dhana kwamba viongozi wa Mlima Kenya ndio walichochea fujo hizo. Kampeni hizo zilitajwa mata 4,360 na kusomwa mara 153,000 huku zikidai Bw Gachagua na wabunge kadhaa kutoka Mlima Kenya ni “makamanda wa fujo.” Ilidaiwa kuwa maandamano hayo hayakutokana na kilio cha umma kuhusu changamoto mbalimbali za kimaisha na kiuchumi. Akaunti 39 zilizohusika na kampeni hii pia zilihusika katika kampeni sambamba kupitia hashtegi #FinancersOfChaos , iliyolenga viongozi wa mashirika ya kijamii na wanahabari. Hii ilionyesha kuwa kulikuwa na mtandao wa washambuliaji waliolenga wanasiasa mbalimbali. Japo mwanzoni kampeni hiyo iliendeshwa katika mtandao wa X ilipanua mawanda yake hadi mtendao wa Facebook. Hashtegi #FinancersOfChaos iliwekwa mara 10 na kusomwa na watu 17, 288 huku zikijibiwa mara 338. Kampeni hizi zilidai kuwa wanaharakati na mashirika ya habari yalifadhili na watu kutoka nje ili kuendelea fujo wakati wa maandamano na vitendo vingine vya uvunjaji sheria.