MAHAKAMA imetoa uamuzi kumtangaza kuwa amekufa, mwanamume aliyetoweka kwa miaka 17 bila kuwasiliana na familia wala jamaa zake. Mahakama Kuu ya Milimani, Nairobi, ilimtangaza Joseph Macharia Karanja kuwa amekufa baada ya kupata kwamba ushahidi uliowasilishwa umeonyesha kuna sababu tosha za kuamini alifariki. “Imetangazwa kwamba Bw Karanja, ambaye alionekana mara ya mwisho Januari 15, 2008, anadhaniwa amekufa kwa madhumuni yote ya kisheria,” mahakama ilisema. Mahakama ilitegemea Kifungu cha 118A cha Sheria ya Ushahidi, kinachoruhusu mahakama kutangaza mtu kuwa amekufa kisheria endapo hakuonekana au kusikika kwa angalau miaka saba. Mahakama pia ilifafanua tarehe ya kifo itakayorekodiwa kwenye cheti cha kifo. Imebainika kuwa kuweka tarehe ya kifo siku Karanja alipotea kungepingana na simu aliyopiga siku tatu baada ya kupotea na ripoti za polisi zilizoonyesha alikuwa “akiendelea kuzunguka.” Vilevile, kuweka tarehe mwishoni mwa kipindi cha miaka saba kungeonekana kinyume cha kawaida. “Hadi mahakama itoe uamuzi, mhusika anadhaniwa kuwa hai. Ni uamuzi huu unaopinga dhana ya uhai. Kwa madhumuni ya Cheti cha Kifo, tarehe ya kifo itachukuliwa kuwa tarehe ya uamuzi huu, au kwa hiari ya Msajili wa Kuzaliwa na Kifo inaweza kurekodiwa kama ‘Haijulikani’ au ‘Inadhaniwa kuanzia’,” mahakama ilisema. Uamuzi huu ulitokana na ombi lililowasilishwa mahakamani na mkewe, Bi Mary Gathoni, mnamo Novemba mwaka uliopita, akiomba kutolewa kwa uamuzi wa kisheria wa kifo cha Bw Karanja na cheti cha kifo. Bi Gathoni aliaambia mahakama kuwa yeye na Karanja walioana mwaka 1989 na walikuwa na watoto wawili. Familia yao ilikuwa ikiishi eneo la Buru Buru Farmers, Ruai, Kaunti ya Nairobi, ambapo Karanja alikuwa akifanya kazi na kuwalea jamaa zake. Kwa mujibu wa Bi Gathoni, mumewe aliajiriwa katika kampuni moja eneo hilo kama katibu na akiwa na ratiba ya kawaida ya kuenda kazi Jumatano. Alisema alimwona mwisho Karanja Januari 15, 2008, alipokuwa akienda kuchukua gari kutoka kwa rafiki yake. “Hakurudi nyumbani siku hiyo,” Bi Gathoni alisema. Baada ya siku mbili, alianza kumtafuta, akitembelea mahali pa kazi na kuwajulisha wasimamizi kwamba mumewe alikuwa amekwenda Umoja na hakurudi. Siku ya tatu, Karanja alimpigia simu kutoka namba binafsi, akisema anataka kurudi nyumbani na kuzungumza na binti yake. Hii ilikuwa mawasiliano yake ya mwisho. Bi Gathoni aliripoti kupotea kwake katika kituo cha polisi cha Ruai, akashirikisha wapelelezi Kayole, akamjulisha ndugu zake nane, akaripoti kwa mkuu wa eneo, na kutembelea hospitali na makaburi bila mafanikio. Polisi walishindwa kumpata licha ya taarifa za awali kuwa alikuwa “akiendelea kuzunguka.” Mahakama ilibaini kuwa vigezo vya Kifungu cha 119 cha Sheria ya Ushahidi vilitimia. “Kwenye mtihani wa uchunguzi, swali ni kama mlalamishi alitafuta mumewe kwa kutosha. Jibu ni ndiyo!” mahakama ilisema. Kwa zaidi ya miaka 16, Karanja hakurudi nyumbani, hakuwa na mawasiliano na familia yake, wala kusimamia mali zake tatu, jambo lililosababisha mahakama kumtangaza kudhaniwa amekufa.