WAKAZI wa Kaunti 13 ikiwemo Nairobi na sehemu nyingi za Ukanda wa Bonde la Ufa, Nyanza na Pwani watapokea mvua ya kadri na nyingi leo, Desemba 29 na kesho Desemba 30, 2025, Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa imesema. Kaunti hizo ni Migori, Homa Bay, Kisii, Narok, Kajiado, Makueni, Machakos, Nairobi, Kericho, Bomet, kusini mwa maeneo ya kaunti za Kitui, Taita Taveta na Kwale. Naibu Mkurugenzi wa Idara hiyo Kennedy Thiong’o alisema mvua ya kesho itakuwa nyingi lakini itapungua jinsi ambavyo siku inavyoendelea. Bw Thiongó alisema wataendelea kutathmini hali na kutoa ushauri iwapo kuna hatari zozote zinazonukia ili msaada utolewe. Mvua inayoshinda mililita 20 ndani ya siku 24 ilishuhudiwa kusini mashariki mnamo Desemba 27. Mvua hiyo ilikuwa ikitarajiwa kupanda hadi zaidi ya mililita 30 ndani ya saa 24 na kuenea maeneo mengine kutoka Desemba 28 hadi Desemba 29. Maeneo hayo ni mashariki, maeneo ya juu ya Bonde la Ufa, Ukanda wa Ziwa Viktoria na sehemu ya chini ya ukanda wa Pwani. Asasi za kupambana na majanga ya dharura yamewekwa ange na mvua hiyo inakuja baada ya ukame ulioanza kushuhudiwa kutokana na kukosekana kwa mvua fupi kuanzia Oktoba-Desemba.