UKARABATI wa uwanja mdogo wa ndege wa Daba huko Tana River unakaribia baada ya jamii kukubali mradi huo . Gavana Bw Dhadho Godhana, ambaye alikutana na wataalam wa Jamii ya Daba, ili kujadiliana kuhusu ukarabati na upanuzi wa uwanja huo wa ndege alisema mradi huo unalenga kufungua maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo. Gavana Godhana alisema aliamua kufanya mkutano huo uliowahusisha wataalamu, vijana, Baraza la Wazee la Kaunti na wafanyakazi wa serikali ya kaunti, ili kuafikiana kuhusu mradi huo. “Lazima tushirikiane kama jamii ili kuendeleza miradi ya maendeleo,” alisema Gavana huyo. Bw Omar Guyo, ambaye aliwakilisha wataalam wa Jamii ya Daba aliomba msamaha kwa niaba ya jamii yake kwa kupinga mradi huo hapo awali. Alisema hapo awali walikuwa hawaelewi kikamilifu umuhimu wa kutenga ardhi kwa ajili ya upanuzi wa uwanja huo wa ndege. Vile vile alikiri kuwa upinzani wa awali ulichochewa pakubwa na habari potovu. Gavana aliwasihi jamii za kaunti hiyo kukumbatia miradi ya maendeleo. “Msichukulie upinzani kama kikwazo cha maendeleo, bali inasaidia katika majadiliano na makubaliano. Ni kupitia ushirikiano wa wazi ndipo tunajenga uaminifu na kusonga mbele kwa pamoja. Lazima tuwe na uwazi kuhusu miradi ya maendeleo,” alisema Gavana huyo. Gavana alisisitiza umuhimu wa maendeleo kama vile miundombinu ya kisasa ili kuvutia uwekezaji wa serikali na sekta za kibinafsi. Aliwahimiza vijana kukumbatia elimu ili wawe na ujuzi utakao wasaidia kupata nafasi za ajira kwenye miradi hiyo. “Vijana ndio watakaonufaika wa kwanza kwenye mradi huu wa ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho cha ndege,” akasema Bw Gavana.