Jirongo kuzikwa leo DCI wakisisitiza hakuuawa: Wafuasi wasema ‘atazikwa na tochi’

MAAFISA wanaochunguza kifo cha mwanasiasa Cyrus Jirongo atakayezikwa leo, wamependekeza uchunguzi wa umma ufanywe baada ya kubaini kuwa hakuna ushahidi wowote wa mauaji katika ajali iliyosababisha kifo chake. Uamuzi huo ulifikiwa baada ya wachunguzi kuondoa uwezekano wa mauaji, wakisema matokeo yao hadi sasa yanaonyesha kifo hicho kilitokana na ajali ya barabarani. “Kulingana na ushahidi uliokusanywa hadi sasa, hakuna lolote linaloonyesha kuwa Jirongo aliuawa,” wachunguzi walisema katika mapendekezo yao kwa Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Mohammed Amin. Awali, Bw Amin alifichua kuwa wachunguzi walizungumza na abiria waliokuwa wamesafiri katika gari aina ya probox lililonaswa na CCTV usiku huo katika eneo la ajali, na kubaini kuwa gari hilo halihusiani na kifo chake. “Hadi sasa, uchunguzi unaonyesha kuwa kifo kilitokana tu na ajali ya barabarani,” Bw Amin alisema kwenye ujumbe uliochapishwa kwenye mitandao ya DCI. Bw Jirongo alifariki asubuhi ya Desemba 13 baada ya gari lake kugongana na basi la abiria karibu na Karai, barabara ya Nairobi–Nakuru, Kaunti ya Nakuru. Alikuwa anaendesha peke yake na kufariki kutokana na majeraha yanayohusiana na ajali, polisi walisema. Chanzo kilichofahamu uchunguzi ulivyofanyika kiliiambia Taifa Leo kuwa DCI tayari wamehoji zaidi ya watu 20, wakiwemo dereva wa basi, kondakta, abiria mmoja wa basi, wafanyakazi wa vituo vya mafuta, na abiria watatu waliokuwa wamesafiri katika Probox iliyotajwa. Licha ya matokeo ya polisi, mjadala umeendelea kuibuka kabla ya mazishi ya waziri huyo wa zamani huku wazee wakiendelea kupinga na kutaka azikwe na kurunzi kaburini kulingana na imani za kitamaduni za jamii ya Watiriki kufichua siri iliyozunguka kifo chake.