Uteuzi wa Mwakwere kama msemaji wa Wamijikenda wakosolewa na viongozi

SIKU kadhaa baada ya sherehe ya kumteua waziri wa zamani Chirau Ali Mwakwere kama msemaji rasmi wa Jamii ya Wamijikenda, kumeibuka upinzani mkali, viongozi na wakazi wakisema mchakato kamili wa uteuzi haukufuatwa. Kwa mujibu wa viongozi kadhaa wa jamii hiyo, sherehe iliyoandaliwa eneo la Vishakani eneobunge la Kaloleni, haikufuata utamaduni, mchakato unaofaa na iliwatenga washikadau wakuu. Mwenyekiti wa Muungano wa Taireni ya jamii ya Wamijikenda Bw Peter Ponda, alidai kuwa uidhinishaji huo ulilenga kuwafaidi watu wachache na si jamii nzima. “Sisi tunataka Umoja wa Wamijikenda. Kile tunachotaka ni taratibu zinazopaswa kumteua kiongozi wetu. Watu wengi hawajahusishwa ni kama watu wachache walikaa wakamteua kiongozi bila kuwahusisha,” akasema Bw Ponda. Kwa mujibu wake, sherehe hizo za utawazo ziliwatenga viongozi wengi waliochaguliwa kutoka jamii hiyo, na hata wale wa kidini na kuibua shaka kuhusu uhalali wake. Alidai kuwa, Bw Mwakwere hakuwa amefanya vya kutosha ili kutajwa kama kiongozi wa jamii hiyo yenye jamii ndogo tisa. “Hauwezi kubalika ukitoka nyumbani uwekwe juu. Marehemu Karisa Maitha alitambuliwa kigogo wa Pwani, si kwa sababu alisema ateuliwe bali ni kwa sababu ya kupigania haki ndio jamii ikamfuata,” akasema Bw Ponda. Kaimu mwenyekiti wa Muungano wa Wamijikenda eneo la Pwani Patrick Mwalimu Rasi, alisema kuwa tamaduni zinazohitajika kabla ya kiongozi wa hadhi hiyo kuidhinishwa hazikufuatwa. Aliongeza kuwa Bw Mwakwere atatambuliwa kama kiongozi rasmi, pindi tu tamaduni hizo zitakapofanyika. “Kitu kinachohusu umijikenda ni lazima kihusishe sala za Kimijikenda, hiyo ndiyo baraka ya jamii. Lakini kuapishwa na wakili ni maslahi ya wanachama wachache. Kuna wazee wa miji tisa ambao wanapaswa kukubali kabla ya hatua hiyo kutambulika,” akasema Bw Rasi. Bi Josephine Charo kutoka kwa muungano huo, alieleza kuwa sherehe hiyo haikuwajumuisha wakazi. “Huyu hata kufika hapa ajitambulishe kwa watu wamjue hakufanya. Kiongozi anatoka kwa Mungu si kwa watu wachache. Hata kuwaambia jamii sherehe inafanyika hawakuwaambia,” akasema Bi Charo.